KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA CHAKULA SALAMA DUNIANI , TBS WASISITIZA UZINGATIAJI WA KANUNI BORA KATIKA UANDAAJI WA CHAKULA .
Na Mwandishi Wetu.
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) kutumia Jukwaa la Biashara la Viwango (Viwango Business Forum) litakalofanyika Juni 5, 2026 katika ukumbi wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam, kuadhimisha Siku ya Chakula Salama Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Juni 7.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 2, 2026 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja wa Tathmini ya Vihatarishi katika Chakula wa TBS, Immaculata Justine, amesema jukwaa hilo litatoa fursa kwa wadau kujadili umuhimu wa usalama wa chakula katika kulinda afya za wananchi pamoja na kukuza biashara ya chakula nchini.Amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo, “Kutoka katika changamoto kuelekea suluhisho: Chakula salama kila mahali,” ambayo inalenga kuhamasisha jamii na wadau kutumia changamoto zilizowahi kujitokeza katika masuala ya usalama wa chakula kama msingi wa kupata suluhisho endelevu.
"Chakula salama ni kile kilichoandaliwa kwa kuzingatia kanuni bora za uandaaji na kutumika kwa namna iliyokusudiwa bila kusababisha madhara kwa mlaji". Amesema.
Amefafanua kuwa kanuni bora za uandaaji wa chakula zinajumuisha masuala mbalimbali muhimu yanayolenga kuhakikisha vihatarishi haviingii kwenye chakula, huku akibainisha kuwa vihatarishi hivyo vinaweza kujumuisha vimelea vya magonjwa kama bakteria, virusi na ukungu ambavyo huweza kuathiri afya ya mlaji.
Aidha, amesema ni wajibu wa kila mdau katika mnyororo wa chakula kuhakikisha chakula kinalindwa dhidi ya vihatarishi kwa kuzingatia kanuni bora katika kila hatua, kuanzia uzalishaji shambani, usafirishaji, uandaaji wa chakula hadi usafi wa mazingira ya chakula.
Amesisitiza kuwa matumizi ya kanuni bora za kilimo, usafirishaji, uandaaji wa chakula na usafi ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata chakula salama na kulinda afya ya jamii.
Reviewed by Adery Masta
on
June 03, 2026
Rating:

No comments: