test

JAMII YAASWA KUWALINDA WATOTO

 


​Jamii imekumbushwa kuwalinda watoto kwa kuwawekea mazingira salama ya kuishi, kupata mahitaji muhimu sambamba na kufundishwa uzalendo kwa Taifa lao.



​Hayo yamejiri Mei 19, 2026 wakati wa utolewaji wa elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi Pamba A, B na C kata ya Mabatini, wilaya ya Nyamagana na shule za Msingi Isenga A, B na Jamhuri zilizopo kata ya Pasiansi, wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza.


​Elimu hiyo mahususi kwa wanafunzi imetolewa na Mkuu wa Polisi Jamii mkoa wa Mwanza ACP Lwelwe Mpina na maafisa kutoka kamisheni ya Polisi Jamii Makao Makuu Dodoma wakiongozwa na SP Daktari Ezekiel Kyogo.


​Akitoa elimu hiyo, ACP Mpina amesema watoto ni Taifa la kesho hivyo amehimiza kuendelea kutunza amani na kuwalea watoto katika misingi bora.


​"Hatuwezi kuwaacha watoto wetu waharibike, hatuwezi kuwaacha watoto wajiingize kwenye utumiaji wa dawa za kulevya na mmomonyoko wa maadili," amesema Mpina.


​Kwa upande wake SP Daktari Ezekiel Kyogo amewataka watoto kuwa wazalendo kwa kuipenda nchi yao Tanzania na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani.


​"Uzalendo ni hali ya kuipenda nchi yako kwa moyo wa dhati, kuilinda na kuitetea. Mzalendo yuko tayari kufa kwa ajili ya kuitetea nchi yake," amesisitiza SP Kyogo.


​Naye Mkaguzi Msaidizi wa Polisi A/Insp Jofrey Mapunda amekemea vitendo vya ukatili kwa watoto na kuwataka wasikubali kurubuniwa ili waweze kufikia ndoto zao.


​Aidha, amewataka watoto wasikubali kushikwa sehemu zao za siri na wakimbaini mtu mwenye tabia mbaya watoe taarifa Polisi mara moja ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.


​Baadhi ya wanafunzi wamesema elimu iliyotolewa na Jeshi la Polisi inaenda kuwasaidia kuwa wazalendo kwa nchi yao na kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia.


​"Ukatili mara nyingi unatokea kwa watoto wadogo na unafanywa na ndugu wa karibu na watoto huogopa kusema. Tumejifunza sehemu sahihi za kupeleka taarifa za uhalifu," amesema Mariam Deus, mwanafunzi wa shule ya Pamba C.


​"Kwa kweli mimi nimejifunza uzalendo kuwa ni kuwapenda wenzangu, nchi yangu, kuwa na utu na kuheshimu wakubwa na wadogo," amesema Daniel Maiko, mwanafunzi wa shule ya Msingi Pamba.



JAMII YAASWA KUWALINDA WATOTO JAMII YAASWA KUWALINDA WATOTO Reviewed by VISION MEDIATZBLOG on May 20, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.