Mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Amina Shabani (21), Mkazi wa Kata ya Muungano Wilaya ya Chato Mkoani Geita, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumfukia Mtoto wake mchanga wa jinsia ya kike akiwa hai ndani ya shimo muda mfupi baada ya kujifungua.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita SACP, Safia Jongo amesema Mtuhumiwa anadaiwa kutenda tukio hilo Mei 16, 2026 majira ya saa 9:00 alasiri Nyumbani kwake, masaa machache baada ya kujifungua siku hiyo majira ya saa 4:00 asubuhi, huku tukio likibainika Mei 17, 2026 majira ya saa 1:00 usiku baada ya Wananchi kusikia sauti ya Mtoto mchanga nyuma ya Nyumba ya Mtuhumiwa bila kumuona Mtoto huyo.
Kamanda Jongo amesema Jeshi la Polisi limefika eneo la tukio na kumwokoa Mtoto huyo kabla ya kumfikisha Hospitali ya Wilaya ya Chato kwa ajili ya matibabu na uchunguzi wa kitabibu, hata hivyo Mtoto huyo alifariki dunia Mei 18, 2026 majira ya saa 10:00 alasiri.
Aidha amesema baada ya kutenda tukio hilo, Mtuhumiwa alikimbia na kujificha kwa lengo la kukwepa mkono wa sheria, lakini Jeshi la Polisi limefanikiwa kumbaini na kumkamata akiwa katika harakati za kutoroka kwenda Mkoa jirani.
Kamanda Jongo amesema chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa na uchunguzi ukikamilika Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria, huku Jeshi hilo likitoa wito kwa Wananchi kuimarisha malezi na uangalizi kwa wanawake wajawazito pamoja na waliokwisha kujifungua ili waweze kupata msaada wa haraka wa Kijamii, kisaikolojia na kiafya unaoweza kusaidia kuzuia matukio ya aina hiyo na kuokoa maisha ya Watoto wachanga
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
May 20, 2026
Rating:

No comments: