Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, leo Mei 16, 2026 amemwakilisha Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Mazishi ya Kitaifa ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Botswana, Hayati Festus Gontebanye Mogae, yaliyofanyika Jijini Gaborone.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Kikwete amesema Tanzania inaungana na Serikali pamoja na Wananchi wa Botswana katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kufuatia kifo cha kiongozi huyo mashuhuri wa Bara la Afrika.
Katika hotuba yake, Dkt. Kikwete amesema kuwa wakati wa uongozi wa Hayati Mogae, ushirikiano na uhusiano wa kindugu kati ya Tanzania na Botswana uliendelea kuimarika kwa kiwango kikubwa ambapo akizungumzia mapenzi ya Hayati Mogae kwa Tanzania, Dkt. Kikwete amesema "Hayati Rais Mogae alikuwa rafiki wa kweli wa Tanzania na aliipenda nchi yetu kwa dhati.”
Dkt. Kikwete pia alieleza kuwa Hayati Rais Mogae alikuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha umoja, mshikamano na amani barani Afrika, sambamba na kushiriki kikamilifu katika juhudi mbalimbali za usuluhishi wa migogoro katika mataifa tofauti ya Afrika.
"Napenda pia kueleza kuwa binafsi nilipata heshima ya kufanya kazi na Rais Mogae kwa mara ya kwanza alipokuwa Makamu wa Rais, wakati mimi nikihudumu kama Waziri katika Serikali za Rais Ali Hassan Mwinyi na Rais Benjamin Mkapa. Nilianza kama Naibu Waziri wa Nishati na Madini, baadaye nikawa Waziri wa Maji, Nishati na Madini, kisha Waziri wa Fedha, na tulifanya kazi vizuri sana ndani ya SADC. Baadaye, alipokuwa Rais wa taifa hili kubwa, mimi nilikuwa nikihudumu kama Rais wa nchi yangu pendwa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."
"Rais Mogae alikuwa mtu mzuri kufanya naye kazi. Alikuwa mwenye misimamo, mwadilifu, na siku zote alikuwa akisema kile alichokiamini, lakini kwa upole na heshima.” Amesema Dkt. Kikwete
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
May 16, 2026
Rating:

No comments: