Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daniel Sillo ametimiza ahadi yake ya kugawa mashine ya kudurufu mitihani (Printer) pamoja na Kompyuta Mpakato (Laptops) katika Shule ya Msingi Merr iliyopo Kata ya Qameyu wilayani Babati mkoani Manyara.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, Mhe. Sillo amesema dhamira kuu ya zoezi hilo ni kuendelea kuboresha sekta ya elimu katika Jimbo la Babati Vijijini kwa kutumia mifumo ya kidijitali ili kurahisisha ufundishaji kwa walimu pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa elimu kwa wanafunzi.
Aidha amesema uwepo wa mashine ya kudurufu mitihani utasaidia kupunguza changamoto iliyokuwa ikiwakabili walimu na wazazi, hususan suala la michango ya uchapishaji wa mitihani iliyokuwa ikitolewa mara kwa mara shuleni hapo.
“Tunataka shule zetu ziendane na mabadiliko ya teknolojia ya sasa. Vifaa hivi vitarahisisha kazi za walimu, kuongeza ubora wa elimu na kupunguza adha kwa wazazi,” amesema Mhe. Sillo.
Vifaa hivyo vimepokelewa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Merr, Mwalimu Florian Safari Yaato pamoja na viongozi mbalimbali wa Kata ya Qameyu.
Kwa upande wake Mwalimu Yaato amemshukuru Mhe. Sillo kwa msaada huo akisema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi katika maandalizi ya mitihani, uhifadhi wa taarifa pamoja na matumizi ya TEHAMA shuleni hapo.
Sillo Atimiza Ahadi ya Kuboresha Elimu Shule ya msingi Meri
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
May 18, 2026
Rating:
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
May 18, 2026
Rating:


No comments: