Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba ameipongeza Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Myunga mkoani Songwe kwa ukuaji wake wa haraka na jitihada zake katika kuchochea uchumi wa viwanda katika mkoa huo na nchi nzima.
Kindamba amesema hayo leo katika hotuba yake kama mgeni rasmi katika Duru ya Tatu ya Mahafali ya 16 ya taasisi hiyo katika Kampasi ya Myunga huku Mkuu wa Taasisi hiyo akisema wahitimu hao ni mafundi wenye ujuzi unaohitajika katika sehemu mbalimbali. "Sina shaka kwa kuona kuwa katika kusherehekea mahafali haya DIT Kampasi ya Myunga imeimarika na kuendelea kwa haraka sana katika jitihada za kulikwamua Taifa hili kiuchumi kwa kuzalisha mafundi sanifu na wanasayansi wanaohitajika katika soko la ajira,""Nimejionea juhudi za kukamilika kwa miundombinu mbalimbali kama vile madarasa na mabweni ambavyo vitaongeza udahili wa wanafunzi, uboreshaji wa mbinu za kufundishia na vifaa vya kufundishia katika Taasisi, haya ni maendeleo mazuri niwapongeze kwa juhudi hizo," amesema Kindamba.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema, Serikali ya Mkoa wa Songwe inatambua kwamba DIT Kampasi ya Myunga ina wajibu mkubwa katika kuchangia utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuchachua uchumi na maendeleo ya viwanda kwa kuwa DIT ni kitovu cha Taaluma na Mafunzo ya Uhandisi na Teknolojia.Amesema Serikali ya awamu ya sita inatarajia kutengeneza ajira kwa wahitimu wa vyuo wakati na kuimarisha uchumi kwa maendeleo ya Taifa.
Ameipongeza DIT kwa juhudi nyingi zinazochukuliwa na taasisi hiyo katika kuboresha sifa za watumishi ili wafanye kazi zao kwa umahiri na ushindani wa kimataifa sambamba na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Kwa upande wa wahitimu, Kindamba amewakumbusha kuwa, baada ya kuhitimu mafanikio katika maisha yao hayatategemea tu elimu waliyoipata DIT bali yatatokana pia na jitihada, "mafanikio yenu yatategemea pia jinsi mtakavyotumia elimu hiyo, ninafahamu zipo changamoto nyingi katika kujiajiri lakini muhimu kuliko yote ni nia na uthubutu kwani penye nia pana njia.Naye Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Dkt. Richard Masika amesema Baraza la Taasisi linaendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo katika Taasisi hiyo ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambapo ameishukuru Serikali kwa kuiwezesha DIT kupata miradi mikubwa miwili ijulikanayo kama "Technical Education Labour Market Survey” (TELMS II) na “East Africa Skills for Transformation and Regional Intergration Project” (EASTRIP).
"Taasisi yetu kwa kuwezeshwa na Serikali tumeweza kuimarisha DIT - Kampasi ya Myunga ambapo miundombinu mbali mbali inaendelea kuboreshwa. Tunaendelea kuvutia watumishi kuja kufanya kazi DIT Myunga," amesema Dkt. Masika.Amezitaja changamoto kuwa ni pamoja na uhitaji wa kuongeza maeneo zaidi ya Taasisi hususan katika Kampasi ya Myunga ambapo Taasisi imeanzisha mchakato wa kufanya uthamini wa eneo lililopo katikati ya maeneo yetu haya mawili yenye hati kazi, amesema anaamini kazi hiyo inayofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Momba itakwisha mapema na hatimaye Taasisi kuweza kulitwaa eneo.
"Sambamba na malengo ya uanzishwaji wa Kampasi hii, mojawapo ikiwa ni kutoa mafunzo ya Teknolojia ya Uchimbaji wa madini, ikiwezekana, Taasisi iongezewe eneo linalopakana na Kampasi ya Myunga “Blasting site”, ili kutoa fursa kwa vijana kusoma fani hiyo kwa vitendo," amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi hiyo, Profesa Preksedis Ndomba amesema kwamba, wahitimu wa programu hizo ni mafundi wenye ujuzi unaohitajika sana katika sehemu mbalimbali zikiwemo kwenye shuleni, hospitalini, viwandani na ofisi mbalimbali.
Ameongeza kuwa DIT imekuwa ikiendesha mafunzo yake kiubunifu zaidi kwa kuhusisha mafunzo ya darasani, atamizi za teknolojia (technology incubator) na mafunzo kwa vitendo viwandani (Teaching factory).
"Mafunzo ya kitaalamu yanaendelea kuimarishwa kwa kuendesha mitaala inayokidhi mahitaji ya soko na kuongeza bajeti ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuwashirikisha wanafunzi katika kutatua changamoto za kisayansi na ufundi zinazoikabili DIT na jamii kwa ujumla," amesema Profesa Ndomba.
Katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 107 (ME – 70, KE - 37). Idadi ya wahitimu wa kike ni sawa na asilimia 35.5. Katika kundi hili kuna wahitimu 9 kutoka Kampasi ya Dar es Salaam ambao ni 4 (ME – 3, KE – 1) wa Shahada ya kwanza na Wahitimu 5 (ME – 5), wa Stashahada, ambao hawakuhudhurishwa katika Awamu ya kwanza ya Mahafali yaliyofanyika tarehe 1 Desemba, 2022 katika Kampasi Kuu ya Dar es Salaam.
Aidha, wahitimu 98 kutoka Kampasi ya Myunga (ME - 62, KE – 36). Kati ya hao, jumla ya wahitimu 12 (ME – 6, KE – 6) wakitunukiwa vyeti vya kuhitimu mafuzo ya kozi ndefu. Na wengine 86 (ME – 56, KE - 30) wakitunikiwa vyeti vya kufuzu mafunzo ya miezi nane (8) ya uongozi yanayofadhiliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Katika kozi ndefu, wahitimu 6 (ME – 3, KE – 3) wanatunukiwa vyeti vya Ufundi Stadi katika fani ya Ufundi Bomba (National Vocational Award (NVA) Level II in Plumbing and Pipe Fitting). Wahitimu 6 (ME – 3, KE - 3) wanatunukiwa vyeti vya Ufundi Stadi katika fani ya Ufundi wa mifumo ya teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) (National Vocational Award (NVA) Level II in Information Communications Technology (ICT)).
No comments: