test

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZINDUA RASMI KAMPENI YA " KIJANISHA MAISHA "

  Na Mwandishi Wetu.

Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kufanya mageuzi yanayolenga kuongeza tija katika uzalishaji kwa kuboresha miundombinu ya kilimo Pamoja na teknolojia katika sekta ya kilimo ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmojammoja na taifa kwa ujumla.

Hii ni kutokana na kujenga mazingira wezeshi  kwa wajasiriamli wa kilimo Pamoja na wale wanaojihusisha na biashara za kilimo kwa kuondoa vikwazo vyote na kubuni mbinu mpya zinazoboresha uwekezaji katika sekta hiyo ili kilimo kimkomboe mkulima moja kwa moja.

Hayo ameyasema Naibu Waziri wa Kilimo,  Antony mavunde wakato akimuwakilisha waziri wa kilimo, Hussein Bashe katika hafla ya mkutano wa PASS TRUST na wadau wa kilimo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam ambapo amewataka wadau hao kukilinda kilimo kupitia ubunifu mbalimbali hasa kuchukua hatua zinazokabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

"Mheshimiwa Rais Mama yetu, Samia Suluhu Hassan anataka kuona neno wakulima wadogo linaondoka katika nchi yetu, badala yake tuwe na wafanyabiashara wa kilimo wadogo, kwani kilimo ni biashara. Ndiyo maana mnaona maboresho ya huduma za ugani, maboresho ya sera za kilimo, uanzishwaji wa miradi ya vijana nchi nzima, ruzuku ya serikali katika pembejeo za kilimo zikiwemo mbolea na mikakati mbalimbali tunayoichukua. Yote haya ni kwa ajili ya kuwakomboa wakulima wa nchi yetu." Amesema Mavunde na kuongeza kuwa ,

"PASS wameonesha njia, tuwaungeni mkono kupitia shughuli zetu ili kesho ya kilimo chetu, kesho ya Maisha yetu iendelee kuwa bora Zaidi. Bila kufanya hivyo athari za mabadiliko ya tabianchi zitaathiri maendeleo ya kilimo."

Aidha Mavunde ameziomba benki zote nchini na taasisi mbalimbali zinazofanya kazi na sekta ya kilimo, kuendelea kubuni njia mbadala za kuleta nafuu kwa wakulima nchini ili kuisaidia serikali kufikia malengo ya kujenga uchumi imara wa taifa hili kupitia sekta ya kilimo.

Mavunde amewapongeza PASS Trust kwa juhudi mbalimbali za ubunifu ambao wameendelea kuuchua katika kukabiliana na changamoto za wakulima nchini hasa katika mnyororo wa thamani.

 Pia amewapongeza PASS kwa kuja na ubunifu wa kuhamasisha mageuzi ya kilimo nchini ili kiendane na sera ya uhifadhi wa mazingira kupitia mradi huu wa Ukuaji wa Kijani Shirikishi, yaani Inclusive Green Growth.

"Kwa hakika malengo yenu ni mazuri sana na ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, kwani siku zote amekuwa akisisitiza tujali mazingira yetu."

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Trust, Yohane Ibrahim Kaduma amesema, PASS Trust ina mchango mkubwa katika kuchochea na kuwezesha ukuaji wa kilimo nchini Tanzania huku tukitoa kipaumbele kwa vijana na wanawake ambapo wanawapa dhamana ya mikopo na huduma za maendeleo ya biashara ili kufikia malengo yao.

Akifafanua kuhusu ushirikishwaji wa wadau wengine wa kilimo katika kikao hicho, Mkurugenzi Kaduma amesema wanaamini katika ushirikiano na mashirika mengine yanayohudumia sekta ya kilimo, ndiyo maana wamewaalika wadau wengine wa sekta hiyo kwa ajili ya kujadili na kubainisha njia mbalimbali zinazoweza kusaidia sekta ya kilimo kupitia ajenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi ambayo inalenga kuhimiza ukuaji wa kilimo kwa kujali uhifadhi wa mazingira asilia.

Naye Balozi wa Denmark nchini Tanzania,  Mette Norgaard ameweka wazi kuwa Tanzania na Denmark ni nchi rafiki na ndiyo maana Serikali ya Denmark inafadhili Asasi ya PASS Trust na Agenda ya Ukuaji wa Kijani Shirikishi kama mpango wa kuchochea uchumi stahimilivu na wenye tija kupitia kilimo kinachoendana na mabadiliko ya tabianchi.

 ''Serikali ya Denmark inafadhili PASS Trust ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na maendeleo ya biashara kwa wafanyabiashara wa kilimo nchini Tanzania, imesaidia kwa kiasi kikubwa wakulima wengi ambao wamegawanyika katika makundi matatu, ambayo ni watu binafsi, vikundi na makampuni yanayojihusisha na kilimo kupitia huduma za vifaa na misaada ya kifedha kwa ajili ya kukuza kilimobiashara”, amesema Balozi.

NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZINDUA RASMI KAMPENI YA " KIJANISHA MAISHA " NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZINDUA RASMI KAMPENI YA " KIJANISHA MAISHA " Reviewed by Adery Masta on February 24, 2023 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.