Na Mwandishi Wetu.
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewashauri wenye visima vya maji kuhakikisha maji yanapimwa ili kukidhi ubora na kulinda usalama wa afya zao.
Hayo yamebainishwa Leo Aprili 24,2024 na Afisa udhibiti Ubora (TBS) Bw.Ibrahim Feruzi wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za TBS, Jijini Dar es Salaam.
Amesema wananchi wamekuwa na desturi ya kujitafutia vyanzo vya maji kutokana na uchache wa vyanzo vya maji salama ili kujipatia suluhisho endelevu ambapo changamoto inayojitokeza ni kutokuwa na uhakika wa ubora na usalama wa maji hayo.
Aidha Bw.Feruzi amesema kuwa TBS kupitia maabara zake inapima maji katika maeneo mawili ambayo ni Mikrobiolojia pamoja na kemikali ambapo maabara hizo zina ithibati hivyo majibu yake yanakubalika popote duniani.
Pamoja na hayo ameeleza umuhimu wa wananchi kufahamu usalama na ubora wa maji ili kuepuka maambukizi ya vimelea hatarishi.
"Kuna vimelea hatarishi kama aina mbalimbali za bakteria kama vile salmonella wanaosababisha ugonjwa wa typhoid ambao wengi mnaufahamu, kuna wadudu wanaitwa Vibrio wanaosababisha ugonjwa wa kipindupindu na wadudu wengine wanaoitwa shigella ambao wanasababisha matumbo ya kuhara, uwepo wa wadudu hao unatupatia kila sababu ya kuhakikisha maji yanapimwa na kutibiwa ili kuwa salama"Bw.Feruzi ameeleza.
Vilevile Bw.Feruzi amesema kupimwa kwa maji kunajumuisha vigezo mbalimbali kama kuangalia kiwango cha Oksijeni,kiwango cha tope,tindikali ya madini mbalimbali hasa metali nzito ambapo inasaidia kufanya tathmini ya ubora na usalama wa maji.
"Viwango vya juu vya metali nzito mfano zebaki (Mercury) vinaweza kusababisha athari kubwa za kiafya kama kansa za ngozi,matatizo ya figo,matatizo ya maini na mengineyo"Bw.Feruzi amesema.
Bw.Feruzi amebainisha kuwa Shughuli za kibinadamu katika rasilimali maji zinanaweza kuchangia uchafuzi wa maji ambayo awali yalikuwa salama hivyo ni vema kufanya upimaji mara kwa mara ili kubaini mapema aina ya uchafuzi na kuitatua mapema ili kulinda mifumo ya ikolojia.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano na Masoko , Bi. Gladness Kaseka amesema upimaji wa maji ya kisima kwa matumizi binafsi ni wa hiari ila kwa wale wanaotaka kusambaza kwa ajili ya matumizi ya watu wengi upimaji ni wa lazima ili kulinda afya za watumiaji.
Kaseka ametoa rai kwa wenye visima binafsi na wale wanaosambaza maji kupima kama biashara kuwa na tamaduni za kupima kujihakikisha usalama na ubora wa maji husika ili kuepuka changamoto zozote zinazoweza kujitokeza kwa watumiaji, na muda wa upimaji hadi kupata majibu ni siku 14.
TBS WATOA WITO KWA WANANCHI KUPIMA MAJI YA VISIMA
Reviewed by Adery Masta
on
April 24, 2024
Rating:
No comments: