Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo, amekabidhi gari maalumu la kubeba Wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Bashnet kilichopo Kata ya Bashnet Wilaya ya Babati Vijijini Mkoani Manyara.
Akizungumza Mei 4, 2024 katika hafla fupi ya kukabidhi gari hilo lililotolewa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa hakuna gari la kubebea wagonjwa Wananchi walikuwa wanapata tabu kuwasaidia ndugu zao kuwatoa ngazi za zahanati kwenda kwenye Vituo vya Afya au kuelekea Hospitali Wilaya wakati mwingine kuelekea Hospitali ya Rufaa.
"Mimi na Wananchi wote wa Jimbo la Babati Vijijini na Mkoa mzima wa Manyara tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya kwenye Jimbo letu, ikiwemo Ujenzi wa Vituo vya Afya na Zahanati hivyo niwaombe gari hili litunzwe na lifanye kazi kwa malengo yaliyokusudiwa" alisema Mhe. Sillo
Pia amewahakikishia Wananchi kuwa, ataendelea na juhudi mbalimbali za kuimarisha huduma za sekta ya afya katika Jimbo la Babati Vijijini kama alivyoahidi kipindi cha kuomba ridhaa ya kutumikia Jimbo hilo.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Babati Vijijini Ndg. Philbert Mdaki amesema kuwa, kama Chama chenye dhamana ya kuwatumikia Watanzania kitaendelea kusimamia vema utekelezaji wa Ilani katika kuwaletea Maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati na Diwani wa Kata ya Madunga Ndg. John Noya alisema gari lililokabidhiwa linaenda kusaidia na kuboresha huduma za afya kwa Wananchi wa Bashnet na Kata jirani.
Vilevile Diwani wa Kata ya Bashnet alimshukuru Mhe. Rais kwa kutimiza ahadi yake na kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo kwa kupeleka miradi mbalimbali ambayo imetekelezwa ikiwemo Kituo cha afya cha bashnet ambacho amekipigania mpaka kikajengwa na hatimaye leo wanajipatia gari mpya ya kubebea Wagonjwa kwa kipindi cha muda mfupi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.
No comments: