Na Mwandishi Wetu.
KATIKA kuadhimisha Siku ya Viwango Duniani, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wadau na wananchi kwa ujumla kushiriki katika kuandaa na kutoa maoni wakati kiwango kikiwa katika mchakato wa utengenezaji ili kiwango kinapotangazwa kikidhi mahitaji ya jamii .
Wito huo umetolewa leo Oktoba 28, 2024 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Viwango Duniani.
Dkt. Katunzi amesema Mwaka huu, maadhimisho hayo yalianza kufanyika Oktoba 21 na kilele itakuwa tarehe 30 Oktoba 2024 , ambapo kumekuwa na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuelimisha umma kupitia vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii juu ya umuhimu wa kushiriki katika mchakato wa uandaaji wa viwango vya kitaifa, kikanda na kimataifa; na kutambua mchango wa wadau kushiriki katika utengenezaji wa viwango nchini.
"Ni matumaini yangu kuwa wadau wote katika nafasi zao, wataendelea kusaidia na kutoa uzoefu na taaluma zao kwa kuchangia ipasavyo katika utengenezwaji wa viwango hapa nchini". Amesema Dkt. Katunzi.
Amesema wanatambua juhudi hizo na mchango mkubwa wa kujitolea kuandaa viwango na hatimaye kuhakikisha afya za watanzania na mazingira vinalindwa na pia kukuza biashara.
Aidha amesema kuwa kwa Takwimu wataalamu hawa kwa mwaka huandaa, kupitia na kurejea Viwango zaidi ya 600.
"Kazi hii ya uandaaji viwango hufanywa kwa kujitolea muda wao na kushirikiana na maafisa Viwango na wadau wengine, hakika shirika linatambua mchango wao mkubwa". Amesema
Pamoja na na hayo amesema Mpaka kufikia maadhimisho haya ya mwaka 2024 Tanzania inashiriki kikamilifu katika kamati 46 za kimataifa (ISO Committees) na 141 kwa kufuatilia utendaji wake (observing member), ushiriki huu unaipa fursa nchi yetu kuwa sehemu ya maamuzi katika uandaaji wa matakwa ya bidhaa mbalimbali duniani.
Amesema pamoja na ushiriki huo bado kuna fursa kubwa kwa wataalamu wetu kuchukua nafasi za uongozi katika kamati hizo za kitaalamu ili kuipa nchi yetu nafasi ya kukuza uchumi kwa kushiriki na kuzalisha bidhaa zinazokidhi ubora wa kimataifa.
Hata hivyo Dkt. Katunzi ameeleza kuwa shirika limeandaa mafunzo mahususi kuhusu ushiriki katika uandaaji viwango kimataifa. Mafunzo hayo yatafanyika kwa washiriki wa kamati hizo za kitaalamu siku ya kilele cha maadhimisho haya tarehe 30 Oktoba, 2024.
TBS WATANGAZA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA VIWANGO 2024
Reviewed by Adery Masta
on
October 28, 2024
Rating:
No comments: