Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limewakamata watu 21 kwa tuhuma za ununuzi na umiliki wa vyuma chakavu vinavyodhaniwa kuwa mali za wizi, ikiwemo miundombinu ya serikali na wananchi.
Watuhumiwa hao walikamatwa katika msako maalumu uliofanyika hivi karibuni, ambapo walikutwa na mali mbalimbali kama milango, mageti, madirisha (grill), vibao vya alama za usalama barabarani, mifuniko ya majitaka na misalaba.
Akizungumza leo Mei 12, 2025 katika kikao maalumu na wafanyabiashara wa vyuma chakavu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, amesema kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakihusishwa na ununuzi wa mali za wizi kwa kushirikiana na wahalifu, jambo linalochangia uharibifu wa miundombinu ya taifa.
Kikao hicho kimehusisha majadiliano ya kina kuhusu changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao, ikiwa ni pamoja na njia bora za kuzuia uhalifu katika sekta hiyo. Wafanyabiashara hao wamekubaliana kuunda kikundi maalumu cha mawasiliano kitakachowawezesha kushirikiana na vyombo vya usalama katika kutoa taarifa za uhalifu.
Aidha, wametoa ahadi ya kutoshiriki tena katika ununuzi wa vyuma vya wizi na miundombinu ya umma na kuahidi kuwa wazalendo katika biashara zao, huku wakiahidi kuunga mkono juhudi za Jeshi la Polisi katika kulinda rasilimali za umma na kupambana na uhalifu.
21 MBARONI KWA UHUJUMU MALIMALI ZA SERIKALI NA ZA MAKABURI
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
May 12, 2025
Rating:

No comments: