Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeutaka Umoja wa waendesha Bajaji za mizigo (GUTA) mkoani humo, kutunza amani kwa kutafuta njia sahihi ya kutatua changamoto wanazokutana nazo katika kazi yao.
Hayo yamejiri leo Juni 5, 2025 katika Uwanja wa Polisi Mabatini, wakati Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafugwa alipokutana na madereva hao pamoja na uongozi wao, kusikiliza na kujadili kero walizonazo kwa lengo la kupata ufumbuzi.
Katika mkutano huo, Kamanda Mutafugwa aliwapongeza madereva hao na uongozi kwa mshikamano wao na ushirikiano na Jeshi la Polisi katika kutanzua na kudhibiti uhalifu. Pia, aliwataka kuzingatia sheria za usalama barabarani, hasa kuheshimu misafara ya viongozi, magari ya dharura na watumiaji wengine wa barabara.
Kikao hicho kimetokana na ombi la Umoja wa waendesha Bajaji kuandika barua ya tarehe 03.06.2025 kwa kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza kuomba kufanya maandamano ya amani tarehe 13 Juni,2025 bila kuweka wazi lengo na dhumuni la maandamano hayo ambapo leo wamemueleza Kamanda kuwa wamepandishiwa kodi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa umoja wa madereva wa Bajaji Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Jeremiah, alisema wamepokea ushauri wa Kamanda na watawasilisha barua rasmi kwa Serikali ili kuomba mazungumzo ya marekebisho ya kodi.
"Ulipaji wa kodi ni uzalendo. Tutalipa kodi zote stahiki ikiwa ni pamoja na za maegesho, vibali vya RATRA, bima na zingine halali ili kujenga taifa letu," alisema Jeremiah.
Naye, Ndaki Shigera, mmoja wa madereva, alithibitisha kuwa wameamua kusitisha mpango wa maandamano na kuahidi kuzingatia elimu ya usalama barabarani waliyopewa na Jeshi la Polisi.
Huu ni mwendelezo wa juhudi za Jeshi la Polisi kushirikiana na jamii katika kuimarisha usalama, kwa kutambua kuwa jukumu la kuzuia uhalifu ni la kila mwananchi.
*Kutoka: Dawati la Habari Polisi Mwanza*

No comments: