Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kukamilika kwa Mradi wa Chanzo cha Maji cha Butimba na utekelezaji wa miradi mingine mikubwa katika Jiji la Mwanza, kutahakikisha uwepo wa majisafi, salama na kutosha kwa kuzidi mahitaji hadi mwaka 2050.
Akizindua rasmi Mradi wa Chanzo cha Maji Butimba, wenye thamani ya Shilingi Bilioni 71.6, Rl amesema mradi huo utaboresha kwa kiwango kikubwa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wakazi wa Mwanza na maeneo jirani.
“Nafahamu kuwa mahitaji ya sasa ya maji katika Jiji la Mwanza ni lita milioni 172 kwa siku, na yataongezeka hadi kufikia lita milioni 450 kwa siku ifikapo mwaka 2050,” Rais Dkt. Samia amesema.
“Hivyo, pamoja na chanzo hiki cha Butimba, Serikali imejipanga kuboresha na kupanua chanzo cha Capripoint pamoja na kujenga chanzo kipya cha Kabangaja. Kwa pamoja, miradi hii itaongeza uzalishaji wa maji hadi kufikia lita milioni 504 kwa siku, kiwango kinachozidi mahitaji ya Jiji la Mwanza hadi mwaka 2050,” Rais Dkr. Samia amebainisha.
Amesisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inakuwa ya uhakika, endelevu na inayoendana na kasi ya ukuaji wa miji.
Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Mradi huo umetekelezwa kupitia Rogramu ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Ziwa Victoria, Lake Victoria Water and Sanitation (LVWATSAN) kwa ufadhili wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (European Investment Bank - EIB) na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (Agence Française de Développement - AFD).
Ametoa shukrani kwa Washirika na Wadau wa Maendeleo kwa ushirikiano wao na Serikali katika kuleta maendeleo.
Amesema kupitia programu ya LVWATSAN awamu ya kwanza, miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya namna hii imetekelezwa na kukamilika katika Miji ya Magu na Misungwi Mkoani Mwanza, pamoja na Mji wa Lamadi uliopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu ambao aliuzindua Juni 19, 2025.

No comments: