IMEELEZWA kuwa kutanguliza upendo kwa wagonjwa humwezesha mgonjwa kuwa na faraja katika kipindi ambacho anatibiwa hivyo kufanya dawa anazotumia kuweza kumsaidia kwa haraka kuweza kupona maradhi yanayomsibu.
Wagonjwa wanaopata matibabu katika Hospitali ya SDA Pasiansi wameelezea kupata huduma ya kiwango kizuri huku wakisikizwa kwa upendo na wakilipia matibabu kwa bei rafiki wakati huo huo wanaotumia bima ya afya hawapati vikwazo vyovyote.
Wakizungumza na ZanzibarLeo jana Jijini Mwanza wagonjwa hao walisema.kuwa kuna mahusiano makubwa kati ya mazungumzo ya kumtia moyo mgonjwa na wakati huo huo akinywa dawa kwani hali hiyo huleta faraja kwa mhusika.
Mkazi wa Pasiansi aliyefanyiwa upasuaji katika hospitali hiyo yenye hadhi ya kiwilaya Faustine Malimi alisema alikuwa hana bima hata hivyo amepokelewa na kupata matibabu huku akirunusiwa kulipia taratibu.
Alisema hali hiyo inampa faraja kwa kuona kuwa ameweza anapata matibabu kuokoa maisha yake huku akielezea furaha yake kwa namna wahudumu wanavyomtanguliza Mungu katika masuala yote ya kimatibabu.
Mkurugenzi wa Hospitali ya SDA Pasiansi Dk Mabula Mayongela alisema wanatoa huduma kwa wagonjwa kwa wakati huku wakiwa na wahudumu wa kiroho ambao hupita wodini kila siku kuwaombea wagonjwa waliolazwa bila kujali tofauti ya dini.
"Hospitali yetu ni Taasisi ya dini ambayo tunahudumia kwa malipo na bima kwa wagonjwa wetu hata hivyo tunajitahidi kutowafanya tunaowahudumia kutuona kuwa tunatanguliza fedha mbele bila kujali uhai wao" alisema Dk Mayongela.
Alisema madaktari na wauguzi wanapaswa kuwa na kauli nzuri kwa wagonjwa ili kuwatia moyo wagonjwa na waweze kuona kuwa wanathaminiwa hivyo hali hiyo humfanya mgonjwa kuwa na faraja.
Dk Mayongela alisema kwa vile taasisi hiyo ni ya dini wanamtanguliza Mungu katika huduma zao kwa kutowatoza wagonjwa bei kubwa katika matibabu hivyo kufanya hospitali hiyo kukimbiliwa na watu wote kuanzia wale wenye uchumi mdogo.

No comments: