Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua rasmi kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 katika Jimbo la Ilemela, Mkoa wa Mwanza, ambapo Mgombea Ubunge kupitia CCM, *Kafiti William Kafiti*, amezindua kampeni zake kwa shamrashamra katika uwanja wa Minazi Mitatu, Kata ya Kitangiri.
Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Ndugu *Michael Masanja Lushinge (Smart)*, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, ambae aliwanadi wagombea wa CCM akiwemo Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ilemela, Ndugu *Kafiti William Kafiti*, pamoja na madiwani, huku akiwaomba wananchi kumpa kura za kishindo Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Mhe. *Dkt. Samia Suluhu Hassan*, ifikapo Oktoba 29, 2025.
Katika hotuba yake, Ndugu Kafiti aliainisha vipaumbele atakavyovipa msukumo mkubwa endapo atapewa ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa Ilemela, likiwepo suala la elimu ambapo ameahidi kujenga madarasa na kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Aidha, kuhusu ajira kwa vijana ameahidi kusukuma mbele mikopo rafiki na fursa za kujiajiri ili vijana Wanufaike na fursa zilizopo.
Kwenye michezo ameahidi kujenga na kukarabati viwanja vya michezo kwa ajili ya vijana.
Kwenye miundombinu ameahidi kuboresha barabara za mitaa zinazokwamisha huduma za kila siku.
Kafiti amesisitiza kuwa anataka kuiona Ilemela yenye maendeleo ya kweli yanayogusa maisha ya kila mwananchi, hasa vijana na wanawake.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa chama, wagombea Ubunge kutoka majimbo jirani, pamoja na wa viti maalum waliokuja kumuunga mkono.
Akizungumza kwa niaba ya wagombea ubunge, Mhe *Ng’wasi Kamani* ameipongeza CCM kwa kuendelea kuwaamini vijana na kuwasogeza katika nafasi za maamuzi. Amesisitiza kuwa chama hicho kimejipambanua kuwa chombo cha matumaini kwa Taifa huku akiahidi kushirikiana na Kafiti kuhakikisha kuwa ahadi zote zinazotolewa kwa wananchi wa Ilemela zinatekelezwa kwa kasi, kwa vitendo na kwa tija.

No comments: