Mgombea ubunge Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Evance Mabugo amewataka wananchi kumchagua kuwa mwakilishi wao kwa kuwa ni mkazi wa eneo hilo anayefahamu changamoto zinazowakabili wananchi hao kwa undani.
Ameyasema hayo jijini mwanza wakati akizungumza na wananchi kwenye uzinduzi wa Kampeni katika uwanja wa dampo mkoani Mwanza.
“Amesema kutokana na rekodi yake ya kuwatumikia wananchi wa eneo hilo kwa muda mrefu kama Mwenyeki wa serikali ya mtaa wa Uhuru kwa miaka kumi anao uzoefu wa kufahamu matatizo yanayowakabili wananchi wa nyamagana .”
Mabugo ameogeza kuwa wananchi waishio katika milima mbalimbali katika eneo hilo hawajaweza kupimiwa maeneo yao waishio hatua inayowafanya kushindwa kuwa na hati miliki ya viwanja vyao kwa ajili ya maendeleo yao.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Itikadi, Mafunzo na Elimu kwa Umma Taifa, Dorice Mpatili alisema kuwa wametafakari wakaona hakuna haja ya kususia uchaguzi bali wapambane ili kuweza kukiondoa chama cha CCM madarakani kwa kupitia uchaguzi ili kuwaondolea wananchi adha zinazowasibu kwa sasa.
“Sisi tunaingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi ili tutumie wawakilishi wetu bungeni kuleta mabadiliko nchini” amesema Mpatili.
Alisema Jiji la Mwanza linatakiwa kufanywa kuwa kitovu cha biashara kwa Kanda ya Nchi za Maziwa Makuu kwani liko katika mazingira wezeshi kuweza kufikika kwa watu wa mataifa hayo kwa urahisi mkubwa.

No comments: