Na Mwandishi Wetu.
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeshiriki katika Maonesho ya Kwanza ya BRELA na wadau Wake yanayoendelea katika Viwanja vya Mlimani City jijini Dar es Salaam, ambapo Shirika limeendela kutoa elimu kwa wananchi na wajasiriamali kuhusu umuhimu wa uzalishaji na uuzaji wa bidhaa zenye ubora na zinazokidhi matakwa ya Viwango.
Akizungumza katika banda la TBS lililoko kwenye maonesho hayo Afisa Udhibiti Ubora TBS kanda ya Mashariki Bwn. Francis Moshy amesema kuwa wazalishaji wanatakiwa kuzalisha bidhaa zilizokidhi matakwa ya viwango kwani kwa kufanya hivyo taifa litapata nguvu kazi kubwa kwani walaji na watumiaji wa bidhaa hizi hawataathirika na bidhaa hafifu.
Aidha ameongeza kuwa TBS kushiriki katika maonesho haya ya BRELA na wadau wake ni fursa kwa wajasirimali kwani watakapofika katika banda la TBS Wataelezwa taratibu za kupata alama ya ubora ambayo inatolewa BURE ili wazalishe bidhaa bora na salama kwa kuzingatia matakwa ya viwango .
“TBS imetumia maonesho haya kama sehemu ya kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali tunawaeleza jinsi wanavyoweza kuthibitisha ubora wa bidhaa zao bila gharama yoyote suala ambalo litawasaidia kupata masoko ndani na nje ya nchi na pia kuwa na ushindani sawia kwa bidhaa zinazopatikana sokoni, pia Shirika limepata nafasi ya kutoa elimu kwa watumiaji wa bidhaa likiwahimiza kuhusu umuhimu wa kusoma taarifa katika bidhaa ili kuwa na utamaduni wa kujiepusha na bidhaa hafifu.
“TBS imetumia maoesho haya kama eneo la kutoa elimu kwa watumiaji wa bidhaa kwani hawa ndio waathirika wakubwa wa bidhaa hafifu, tumewasisitiza kuhakikisha wanasoma maelezo ya bidhaa husika hususani muda wa matumizi wa bidhaa husika pamoja na nembo ya ubora ili kujihakikishia kuwa bidhaa wanazotumia ni bora na salama " alimalizia Bwn. Moshy.
Kwa upande mwingine mmoja wa wajasiriamali aliyefika kwenye banda la TBS Leo hii katika maonesho haya ya BRELA amelipongeza Shirika kwa Elimu nzuri ya Viwango linayotoa kwa Wazalishaji na Wananchi kwa ujumla.
TBS YAWAFIKIA WAJASIRIAMALI NA WAFANYA BIASHARA MAONESHO YA BRELA
Reviewed by Adery Masta
on
October 27, 2023
Rating:
No comments: