test

MBUNGE WA JIMBO LA NGORONGORO AANZISHA MFUKO MAALUMU WA KUSAIDIA WANAFUNZI.



Wakati serikali ikiendelea kusukuma mbele ajenda ya elimu bure kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita, juhudi hizo sasa zinaendelea kuungwa mkono kwa vitendo na viongozi mbalimbali nchini.




Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, mkoani Arusha Yannick Ndoinyo, ameibuka na mpango maalum wa kuanzisha mfuko wa elimu utakaowanufaisha wanafunzi 280 kutoka wilayani humo sawa na watoto 10 kutoka kila kata  wanaotoka katika familia zisizo na uwezo wa kuwapeleka sekondari.


Hatua hiyo imekuja kufuatia changamoto kubwa ya kipato inayowakabili wakazi wengi wa Ngorongoro, ambao kwa kiasi kikubwa hutegemea ufugaji kama chanzo chao kikuu cha maisha.


Katika kutekeleza azma hiyo, Ndoinyo ameitisha kikao mkaalum kilichowakutanisha wadau wa maendeleo ya elimu, wakiwemo makampuni ya utalii, taasisi za fedha pamoja na mashirika ya umma, kwa lengo la kujadili na kuanzisha rasmi mfuko huo wa elimu.


Lengo kuu likiwa ni kuhakikisha wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari kutoka familia duni wanapata mahitaji muhimu ya kuanzia safari yao ya elimu  bila vikwazo vya kifedha.


“Wazo hili lilianza mwaka 2025 nilipochaguliwa kuwa mbunge. Nilipokea maombi mengi kutoka kwa wazazi waliokuwa na changamoto ya kuwapeleka watoto wao shule.


Nilianza kwa kusaidia wanafunzi 80  wavulana 40 na wasichana 40  na hapo ndipo nikatambua hitaji ni kubwa zaidi.”


Anaongeza kuwa mfuko huo si tu msaada wa vifaa, bali ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa taifa.


Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Mohamed Hussein, akimuwakilisha waziri wa Elimu, amesema serikali tayari imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu.


Ametaja ajira za walimu zaidi ya elfu 20, ujenzi wa madarasa zaidi ya elfu 30 pamoja na mabweni kwa wanafunzi kutoka jamii za wafugaji, kuwa ni sehemu ya juhudi hizo.


“Tunampongeza Mbunge wa Ngorongoro kwa kuunga mkono jitihada za serikali. Huu ni mfano wa utekelezaji halisi wa sera ya elimu na mchango muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa elimu bora.”


Nao viongozi wa wilaya hiyo wameahidi kusimamia mfuko huo kwa uwazi na uwajibikaji wa hali ya juu.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Manja Yaile, amesema watahakikisha kila mchango unamfikia mlengwa aliyekusudiwa.








“Tutahakikisha mfuko unakuwa wa kuaminika. Kila anayechangia ataona matokeo yake kwa wanafunzi wanaonufaika.”


Zaidi ya hapo, mfuko huo unatarajiwa kuwa daraja la fursa kwa vijana ukisaidia pia kuwaunganisha na nafasi mbalimbali kama ufadhili wa masomo kupitia programu kama Samia Scholarship.


Hivyo basi, mfuko huu hauishii kwenye sare, madaftari au vifaa vya shule pekee  bali unapanua wigo wa ndoto kwa vijana wa Ngorongoro.


Katika dunia ya leo, elimu si chaguo  ni silaha na wilaya ya Ngorongoro, kupitia mfuko huu, inaanza kuandaa kizazi kitakachobadilisha simulizi ya kesho.

MBUNGE WA JIMBO LA NGORONGORO AANZISHA MFUKO MAALUMU WA KUSAIDIA WANAFUNZI. MBUNGE WA JIMBO LA NGORONGORO AANZISHA MFUKO MAALUMU WA KUSAIDIA WANAFUNZI. Reviewed by VISION MEDIATZBLOG on March 29, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.