Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara (TANROADS) kumsimamia Mkandarasi kampuni ya Jiangxi Geo Engineering kukamilisha kwa wakati ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Dareda hadi Dongobesh (km 60) sehemu ya kwanza ya Dareda Centre hadi Dareda Missioni (km 7) ili kuufungua kiuchumi Mkoa wa Manyara.
Bashungwa amezungumza hayo Wilayani Babati Mkoani Manyara Aprili 06, 2024 wakati akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo kati ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) na kampuni ya M/s Jiangxi Geo Engineering (Group) Corporation ya China kwa gharama ya Shilingi Billioni 9.88.
“Tumempa Mkandarasi huyu kwa kuwa tayari anatekeleza miradi mingine ya barabara maeneo haya na jirani na tumemuongezea hii nyingine kwa kuwa si kilometa nyingi hivyo Mtendaji Mkuu sitaki kusikia visingizio nataka barabara hiyo ikamilike haraka maana hata Wakandarasi wa ndani kilometa saba wangeweza kuzijenga”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa amemtaka Mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Labay-Haydom (km25) na barabara ya Mbulu-Garbabi (km 25) ambapo Serikali inakwenda kulipa madeni ambayo alikuwa anayadai ili miradi yote iweze kukamilishwa kwa haraka.
Aidha, Bashungwa amem
pongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kwa kutekeleza maagizo ya Wizara ya kutolimbikiza kazi nyingi kwa Mkandarasi mmoja na hivyo miradi mingi kuchelewa na kusababishia hasara Serikali.
“Nikupongeze Mtendaji Mkuu kwa kutumia hatua za kimkataba kumuondoa Mkandarasi wa barabara ya Lukuyufusi - Mkenda Mkoani Ruvuma mara baada ya kuona hafanyi vizuri kwenye maeneo mengine”, amesema Bashungwa.
Bashungwa amempongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kwa kusimamia ushiriki wa Wahandisi Washauri wa ndani katika usimamizi wa miradi ambapo katika mradi huu usimamizi utatekelezwa kupitia Kitengo cha Usimamizi wa Miradi cha TANROADS (TECU).
No comments: