Na Mwandishi Wetu, Dodoma
SHIRIKA la Viwango Tanzania(TBS) limetumia Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa usalama Barabarani kutoa elimu kwa umma ambapo limesisitiza kwamba pamoja na mambo mengine limekuwa likihakikisha magari yote yanayoingia nchini yanakuwa salama na yanachangia kwa kiasi kikubwa usalama barabarani .
Aidha, shirika hilo limesema limekuwa likihakikisha vipuri vinavyoingizwa hapa nchini vinapimwa ubora kulingana na viwango, kwani wakati wote kama vipuri havina viwango vinakuwa chanzo cha ajali.
Hayo yalisemwa wiki iliyopita na Meneja wa Uandaaji wa Viwango wa TBS, Mhandisi Yona Afrika, wakati akieleza majukumu ya TBS na kutoa elimu kwa wananchi waliotembelea banda la shirika hilo kwenye Maadhimisho ya Nenda kwa Usalama yaliyoanza Agosti 26 hadi 30, mwaka huu kwenye kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Akisisitiza zaidi, Mhandisi Yona alisisitiza kwamba; Tukumbuke gari linatumia mafuta, kuna petroli, diseli na gesi, vitu hivyo vyote vinahitaji ubora, ambapo msimamizi wake ni TBS, kwani gari likiwa linazimazima barabarani linaweza kusababisha ajali, kwa maana kwamba mafuta ni machafu, kwa hiyo wale wote watumiaji na waagizaji wote wa mafuta wanajua kwamba ili yaweza kuingia nchini ni lazima yathibitishwe na TBS.
"Bidhaa zote zinazotumika barabarani zinasimamiwa na TBS hadi matuta yana viwango vyake , alama za barabarani zina viwango vyake mpaka zile lami zinazotumika kwenye ujenzi viwango vyake tunaandaa sisi, kwa hiyo mnaweza kuona jinsi TBS tulivyo wadau wakubwa wa usalama barabarani, ndiyo maana tumeshiriki kwenye Wiki ya Maadhimisho ya Nenda kwa Usalama Barabarani.".
Alisema TBS imeshiriki kwenye maadhimisho hayo wakiwa na jukumu kuu la kuandaa viwango vinavyotumika kwenye vifaa (vipuri) mbalimbali kwenye magari, pikipiki za miguu mitatu (Bajaj) pikipiki za miguu miwili na kofia ngumu (Elemet) za waendesha pikipiki.
Akizungumzia pikipiki, Yona alisema zenyewe inabidi zithibitishwe ubora , ziwe zinakidhi vigezo na kwamba vigezo hivyo, vimeainishwa vizuri ambapo zinatakiwa ziwe na kioo cha kuona nyuma (Site mirrow) bila kuathiri nafasi ya pikipiki kupita maeneo mengine.
Aidha, alisema kofia ngumu nazo zina kiwango, ambapo zinatakiwa ziundwe na malighafi ngumu ambazo hazitamuumiza ambaye atavaa kofia iwapo kutatokea tukio la ajali na kichwa kikawa cha kwanza kufika chini.
Alisema malighafi ambazo zinatakiwa kutengeneza kofia hata kama ni za plastiki ziwe na uwezo wa kunyonya athari (impact) na kwamba ndani ziwe na malighafi laini kwa maana ya magodoro yanayozuia kichwa kisikutane na plastiki.
Pia, Yona alisema kofia ya pikipiki inatakiwa kuzuia masikio yasionekane na kwamba kiwango cha chini kabisa cha kofia ngumu wanachoruhusu ni cha robo tatu ambayo inafunika kichwa, masikio hadi chini ya kidevu.
Alitaja kofia ngumu nyingine kuwa ni ile inayofunika kichwa hadi kidefu ambayo inaitwa Full Elemet. Hata hivyo,Yona alisema kofia ngumu zinazoruhusiwa kwa Tanzania ni zile zinazofunika kichwa hadi kidevu na kofia zote mbili zinatakiwa kuwa na uwezo wa kukaa kichwani bila kutoka, iwapo tatizo la ajali litatokea.
Alisema kofia ngumu inayoishia kwenye masikio ni ile ambayo chini kunakuwa na kamba ambayo inafungwa kwa ajili ya kuhakikisha haitoki kwenye kichwa vha mvaaji. "Na ile nyingine ambayo ina kidevu moja kwa moja maana ukifunga inakuja kukamata kwenye kidevu. Mtu haweze kupata madhara ya kwenye kichwa endapo amevaa kofia ngumu kwa usahihi na kofia ngumu sahii.
Sasa haya yote yanaendana kwa kutumia kofia ngumu ambazo zimethibitishwa kwa kutumia kiwango chetuTZS 1478 cha mwaka 2013," alisema. Yona. Alisisitiza kwamba wakati wote pikipiki inatakuwa kuwa na kofia ngumu mbili yaani ya dereva na abiria.
TBS WATOA ELIMU KWA UMMA , MAADHIMISHO YA WIKI YA NENDA KWA USALAMA BARABARANI
Reviewed by Adery Masta
on
September 03, 2024
Rating:
No comments: