Na Mwandishi Wetu
Umoja wa Amani Kwanza Mkoani Pwani, umetoa rai ya Ushirikishwaji wa Watu Wenye Ulemavu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwani ni haki Yao ya msingi.
Katika mkutano uliofanyika Kibaha, Umoja huo umetoa wito kwa vyama vya siasa kuhakikisha wanatoa nafasi kwa watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, Novemba 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 bila ubaguzi.
Umoja huo pia umesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na kuepuka machafuko katika kipindi hicho .
Katibu wa Umoja wa Amani Kwanza Mkoani Pwani, Halima Jumanne Yusuph, alieleza kwamba Katiba inasisitiza usawa wa binadamu, na hivyo ni muhimu kwa vyama vya siasa na jamii kwa ujumla kuwapa nafasi watu wenye ulemavu kushiriki na kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Alikemea vikali vitendo vya ramli chonganishi vinavyolenga watu wenye ulemavu wa ngozi, akieleza kuwa ni muhimu kulipiga vita suala hilo kuelekea uchaguzi.
Katika mkutano huo, Taasisi mbalimbali kama vile Taasisi ya Mwalimu Nyerere na Wazalendo Huru zilishiriki, na kujadili masuala muhimu kama vile uchaguzi na kupinga ukatili dhidi ya watoto na watu wenye ulemavu.
MaryRose Bujash, Mkurugenzi wa Africa Talent Forum, aliomba jamii kutowatenga watu wenye ulemavu, akisisitiza kwamba nao wana uwezo mkubwa wa kushika nafasi za uongozi.
David Mramba, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Pwani, alieleza CCM inatoa nafasi kwa watu wenye ulemavu kushiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii.
"CCM kupitia Serikali tumeweza kushuhudia Rais Samia Suluhu Hassan akitoa nafasi za uongozi kwa makundi maalum bila ubaguzi na Chama Kijumla kimekuwa hakibagui" alisisitiza Mramba.
Mwenyekiti wa Umoja wa Amani Kwanza, Mwarami Mtete, aliishukuru Serikali ya Mkoa wa Pwani pamoja na vyombo vya ulinzi kwa ushirikiano wao katika kufanikisha majukumu ya umoja huo.
No comments: