> Ushirikiano huu mpya waleta mpango wa malipo nafuu ya simu janja katika maduka 63 ya YAS
Dar es Salaam, Tanzania – 27 Juni 2025 – Kampuni ya mawasiliano ya YAS, kwa kushirikiana na Watu Tanzania kupitia huduma ya Watu Simu, imetangaza ushirikiano wenye lengo la kurahisisha upatikanaji wa simu janja kwa wananchi wa kawaida nchini kote. Mpango huu mpya unawawezesha Watanzania kumiliki simu janja kwa malipo nafuu kupitia mtandao wa maduka ya YAS na Mixx Express.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Daniel Nnko, Mkuu wa Kitengo cha Ukuzaji Masoko na Mauzo – YAS alisema:
“YAS tunaamini kila Mtanzania anastahili kuwa na nyenzo za kufanikisha ndoto zake katika ulimwengu huu wa kidijitali. Kupitia ushirikiano huu, tunarahisisha upatikanaji wa simu janja kama nyenzo muhimu itakayowapa Watanzania uwezo wa kutumia mtandao wetu wa 4G na 5G ulioenea kila kona ya nchi. Pia, hatutatoza ada za miamala kwa wateja watakapofanya malipo ya simu janja zao kupitia Mixx, ili kuhakikisha tunajenga Tanzania ya kidijitali ambayo ni jumuishi kwa wote.”
Mpango huu umeanza kutekelezwa katika maduka 63 ya YAS kote nchini, na mpango wa kupanua huduma hii hadi kwenye maduka mengine ya YAS/Mixx Express uko mbioni. Simu za kwanza kupatikana chini ya mpango huu ni Samsung Galaxy A05 na A05s, ambazo zinajulikana kwa ubora na bei nafuu, zikiwa zimebuniwa kukidhi mahitaji ya kila siku ya Mtanzania wa kawaida.
Kwa upande wake, Moses Mtweve, Mkuu wa Kitengo cha Simu – Watu Tanzania alieleza:
“Lengo letu ni rahisi. Tunataka kuhakikisha kwamba simu janja zinapatikana kwa bei nafuu na kwa kila mtu. Kwa kuunganisha mfumo wa mikopo ya simu ya Watu na uwanda mkubwa wa YAS nchini, tutaleta mabadiliko kwa kiwango kikubwa. Ushirikiano huu ni hatua kubwa kuelekea Tanzania iliyo na mawasiliano bora na ujumuishaji wa kifedha.”
Wateja wanaweza kufika katika duka lolote la YAS na kuanza safari yao ya kidijitali kwa kulipa kiasi kidogo cha awali, na kumalizia salio la simu kupitia malipo ya kila siku, kila wiki, au kila mwezi kupitia mfumo wa kidijitali wa Watu.
Kwa upande wa kampuni ya kutengeneza simu, Samsung Tanzania, kupitia Mkuu wa Kitengo cha Simu, Mgopelini Hamza Kiwanga, aliunga mkono ushirikiano huo kwa kusema:
“Samsung tunafurahia kushirikiana na YAS na Watu Tanzania katika kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kutumia teknolojia ya kisasa kupitia simu janja zetu. Galaxy A05 na A05s ni simu madhubuti, nafuu, na zinazokidhi mahitaji ya kila siku – zikitengenezwa kwa ajili ya mazingira halisi ya maisha ya Watanzania. Tunaamini ushirikiano huu utafungua milango ya fursa zaidi kwa kila mmoja.”
Ushirikiano huu unaakisi dhamira ya pamoja ya kampuni zote tatu katika kukuza ujumuishaji wa kidijitali na kifedha nchini Tanzania. Lengo ni kuwahudumia maelfu ya wateja ifikapo mwisho wa mwaka 2025.

No comments: