Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbulu Paulo Bura amewataka Madiwani kwenda kutoa Elimu ya bima ya afya kwa wote kwa wananchi kwenye maeneo wanayotoka.
Hayo yamesemwa leo tarehe 27/01/2026 kwenye Baraza la Madiwani la robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, wakati akitoa salamu za Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mhe.Michael Semindu.
“ Kwanza madiwani wapewe elimu ya kutosha kuhusu bima ya afya kwa watu wote kisha wao waishushe elimu hiyo kwa wananchi wote,mnaweza kuamua kama Halmashauri kuwapa elimu Madiwani na Watendaji wao au Wenyeviti wa Vijiji ili elimu ifike kwa Wananchi.”Alisema Bura
Sambamba na hilo Katibu Tawala aliwataka Madiwani kushirikiana na Watendaji kuhakikisha Wanafunzi wanaripoti Shule hasa wa kidato cha kwanza, kwani kumekua na tabia ya kuwakatisha watoto masomo ili waolewe.
Akizungungumza katika kikao hicho,Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Mhe.Yeconia Maleyecky aliwahimiza watendaji wa Halmashauri kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi, kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kuzingatia sheria,kanuni na miongozo ya serikali katika utekelezaji wa majukumu yao.
Katika kikao hicho, Madiwani walipitia hali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,pamoja na changamoto zilizojitokeza katika robo ya pili. Pia Baraza lilijadili mikakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuhakikisha Halmashauri inatoa huduma bora kwa wananchi.
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
January 27, 2026
Rating:




No comments: