Chuo cha Polisi Wanamaji Tanzania kilichopo jijini Mwanza kimefungua mafunzo maalum kwa wanawake wa Mkoa huo ikiwa ni sehemu ya hamasa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi 2026.
Akifungua mafunzo hayo, Afisa Mnadhimu Namba Moja wa chuo hicho, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhan Sarige, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanawake katika kukabiliana na ajali za majini pindi zinapotokea, huku akisisitiza kuwa elimu hiyo itawasaidia kuwa na uelewa wa mbinu sahihi za uokoaji na namna ya kujilinda wanapokumbana na hatari majini.
ACP Sarige ameeleza kuwa wanawake ni kundi muhimu katika jamii na ana imani kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa kuifikisha elimu hiyo kwa jamii kwa ufanisi zaidi, hivyo kusaidia kupunguza ajali na madhara yatokanayo na matukio ya majini.
Aidha, amebainisha kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana ni Msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira 2050.” ambapo amebainisha kuwa Kauli mbiu hiyo, inaakisi dhamira ya kuwapa wanawake nafasi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uelewa na ushiriki wa wanawake katika masuala ya usalama majini, sambamba na kuhamasisha usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
March 02, 2026
Rating:


No comments: