Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Mwanza, SSP Ibrahim Sunday, ametoa rai kwa madereva wa pikipiki za magurudumu matatu (Bajaji) za abiria kuzingatia na kufuata sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.
Akizungumza na mamia ya madereva waliojitokeza katika uwanja wa Polisi Mabatini kupata elimu ya usalama barabarani, SSP Sunday amewataka madereva hao kuendelea kutii sheria bila shuruti.
"Tumekuwa na madereva wa bajaji ambao kimsingi hawatambui matumizi sahihi ya barabara. Dereva anaona kana kwamba anatumia barabara ya kwake peke yake, jambo ambalo si sawa kwani linaweza kusababisha ajali," alisema SSP Sunday.
Aidha, SSP Sunday aliongeza kuwa operesheni inayoendelea hivi sasa inaenda sambamba na utoaji wa elimu kuhusu masuala ya usalama barabarani. Alisisitiza kukomesha tabia hatarishi zinazofanywa na madereva hao:
"Kuna kosa ambalo mmeendelea kulifanya, ambalo kwa neno maarufu ninyi mnaliita 'kuchora'. Hii si sawa, na ukibainika hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yako."
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa waendesha Bajaji mkoani Mwanza, Mansour Ahmada Selemani, amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani humo kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuendelea kutoa elimu hiyo. Alieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia wanapokuwa barabarani ili kuzingatia sheria zilizowekwa.
Naye Imaculata Godfrey, mmoja wa madereva wa bajaji, amepongeza hatua hiyo akisema kuwa itawasaidia kuwaelimisha wenzao ambao hawakupata nafasi ya kuhudhuria mafunzo hayo.
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
April 02, 2026
Rating:







No comments: