test

SERIKALI YAIPONGEZA DIT , KUPATA CHETI CHA KIMATAIFA CHA ISO 21001:2018

Na Mwandishi Wetu.

SERIKALI imeeleza kuwa hatua ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kupata cheti cha kimataifa cha ISO 21001:2018 ni chachu muhimu katika kuunganisha elimu ya ufundi na mahitaji halisi ya sekta ya viwanda nchini.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi cheti hicho iliyofanyika Kampasi kuu jijini Dar es Salaam leo Aprili 10, 2026 kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Hussein Mohamed Omar amesema mafanikio hayo yanaonesha namna Serikali  inavyolenga kuifanya elimu iwe chombo cha kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi wa moja kwa moja kwa viwanda.

Amesema Serikali imekuwa ikiwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu ili kuhakikisha wahitimu wanakuwa na maarifa yanayokidhi mahitaji ya uzalishaji, teknolojia na ubunifu unaohitajika katika uchumi wa kisasa.

“Lengo la Serikali si kutoa elimu ya vyeti pekee, bali elimu inayojenga ujuzi wa vitendo. Hii itawasaidia vijana kujiajiri, kuajiriwa na kushiriki moja kwa moja katika kukuza sekta ya viwanda na uchumi wa taifa,” amesema Hussein.


Ameongeza kuwa mafanikio ya DIT yanaakisi umuhimu wa kuoanisha mitaala ya elimu na mahitaji ya soko la ajira, hasa katika nyanja za teknolojia na uzalishaji, ili wahitimu wawe tayari kuingia kwenye mifumo ya viwanda bila changamoto kubwa.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la taasisi hiyo, Mhandisi Dkt. Richard Masika amesema kupatikana kwa cheti hicho ni matokeo ya maboresho ya muda mrefu yaliyolenga kujenga mfumo imara wa elimu unaoendana na mahitaji ya viwanda na maendeleo ya taifa.


Ameeleza kuwa maboresho hayo yaliyoanza mwaka wa fedha 2021/22 yamelenga kuhakikisha wahitimu wa DIT wanakuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji, ubunifu na ushindani wa kimataifa.

Masika amesema cheti hicho kinahusu kampasi zote tatu za taasisi hiyo ambazo ni Dar es Salaam, Mwanza na Songwe, na kwamba kitaongeza uaminifu kwa wadau wa viwanda pamoja na kuongeza ushindani wa wahitimu katika soko la ajira.


Ameongeza kuwa hatua hiyo pia inaunga mkono utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2023 pamoja na dira ya maendeleo ya taifa ya Tanzania Development Vision 2050 inayolenga kujenga uchumi wa viwanda unaotegemea rasilimali watu wenye ujuzi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango (TBS), Dkt. Ashura Katunzi amesema utoaji wa cheti hicho unaonesha kuwa DIT imekidhi viwango vya kimataifa katika usimamizi wa elimu, jambo linaloifanya kuwa taasisi ya mfano katika kuandaa wataalamu wa kuhimili ushindani wa soko la dunia.

Amesema cheti hicho ni uthibitisho wa ubora wa mifumo ya elimu inayotolewa na taasisi hiyo na kinaimarisha nafasi ya wahitimu wake katika sekta ya viwanda na teknolojia.



SERIKALI YAIPONGEZA DIT , KUPATA CHETI CHA KIMATAIFA CHA ISO 21001:2018 SERIKALI YAIPONGEZA DIT , KUPATA CHETI CHA KIMATAIFA CHA ISO 21001:2018 Reviewed by Adery Masta on April 11, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.