Na Mwandishi Wetu.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuonesha dhamira yake ya kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa na kusindikwa nchini zinakidhi viwango vinavyotakiwa kwa kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya 29 ya Wiki ya Maziwa nchini yanayofanyika katika Viwanja vya Mwembetogwa mkoani Iringa.
Maadhimisho hayo yaliyoanza Mei 25 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 1, 2026, yamewakutanisha maelfu ya wadau wa sekta ya maziwa kutoka ndani na nje ya mkoa wa Iringa, wakiwemo wafugaji, wasindikaji, wafanyabiashara, taasisi za serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Kwa mwaka huu, maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo "Rasimisha Biashara ya Maziwa, Okoa Maisha ya Walaji, Ongeza Kipato, Changia Uchumi," ambayo inalenga kuhamasisha uzalishaji, usindikaji na biashara ya maziwa inayofuata sheria, kanuni na viwango vya ubora ili kulinda afya za walaji na kukuza uchumi wa taifa.
Katika maonesho hayo, TBS imekuwa ikitoa elimu kwa wasindikaji wa maziwa, hususan wale wa ngazi ndogo, kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango katika hatua zote za usindikaji wa maziwa na bidhaa zake. Elimu hiyo imejikita katika mbinu sahihi za usafi, matumizi ya vifaa vinavyokidhi viwango, uhifadhi wa maziwa pamoja na taratibu za kupata alama ya ubora ya TBS.
Maafisa wa TBS wameeleza kuwa changamoto kubwa inayowakabili baadhi ya wasindikaji wadogo siyo ukosefu wa nia ya kuzalisha bidhaa bora, bali ni upungufu wa elimu kuhusu mahitaji ya viwango na taratibu za uthibitishaji wa ubora. Kutokana na hali hiyo, shirika hilo limeamua kutumia jukwaa la Wiki ya Maziwa kuwafikia wadau wengi zaidi na kuwajengea uwezo unaohitajika ili kuboresha ushindani wa bidhaa zao sokoni.
Ushiriki wa TBS katika maadhimisho hayo umepokelewa kwa hamasa kubwa na wadau wa sekta ya maziwa, huku wengi wakitumia fursa hiyo kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu viwango, usalama wa chakula na taratibu za kupata alama ya ubora ambayo imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kujenga imani kwa walaji.
Wadau wa sekta hiyo wameeleza kuwa elimu inayotolewa na TBS itasaidia kuongeza uzalishaji wa bidhaa salama na zenye ubora, jambo litakalowezesha wasindikaji kupanua masoko yao ndani na nje ya nchi sambamba na kuongeza kipato chao.
Aidha, maadhimisho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujifunza teknolojia mpya za uzalishaji na usindikaji wa maziwa pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wa sekta hiyo. Hatua hiyo inatajwa kuwa chachu ya kukuza mnyororo mzima wa thamani wa maziwa nchini na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi.
Kupitia ushiriki wake katika Wiki ya Maziwa 2026, TBS imeendelea kuthibitisha nafasi yake muhimu katika kuhakikisha bidhaa za maziwa zinazowafikia walaji zinakuwa salama, bora na zinazokidhi viwango vinavyotambulika, huku ikiendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo kwa wazalishaji na wasindikaji wa maziwa nchini.
Reviewed by Adery Masta
on
May 31, 2026
Rating:




No comments: