test

HALMASHAURI YA WILAYA YA NGORONGORO KUENDELEA KUUNGA MKONO MIRADI YA WANANCHI, YAUNDA KAMATI MAALUM YA MAPATO

 

NGORONGORO, Juni 5, 2026 


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mhe. Manja Sironga Yaile, amesema halmashauri hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za wananchi wa kata mbalimbali wilayani humo wanaoanzisha na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa nguvu zao wenyewe.



Mhe. Yaile alitoa kauli hiyo leo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro uliolenga kujadili utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Katika hotuba yake, aliwataka madiwani kuendelea kuhamasisha wananchi kuchangia na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao. Aidha, aliwapongeza wananchi kwa juhudi wanazoendelea kuzifanya katika ujenzi na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji, utunzaji wa mazingira na nyinginezo.


Akizungumzia suala la mapato, Mhe. Yaile alisema kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, halmashauri imekusanya jumla ya shilingi 3,191,060,180 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato, kiasi kinacholingana na asilimia 77 ya makisio ya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026.




Ili kuhakikisha lengo la ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 100 linafikiwa, Mwenyekiti huyo alitangaza kuundwa kwa Kamati Maalum ya Ufuatiliaji wa Mapato ambayo halmashauri ilipaswa kuyapata lakini haijayapata kwa muda mrefu, ikiwemo mapato yatokanayo na tozo ya huduma (Service Levy).

Kamati hiyo itaundwa na wajumbe saba kutoka Baraza la Madiwani watakaoshirikiana na wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Kwa mujibu wa Mhe. Yaile, jukumu kuu la kamati hiyo litakuwa kufuatilia mapato yanayostahili kulipwa kwa halmashauri kutoka kwa mamlaka, taasisi na makampuni mbalimbali yanayoendesha shughuli za kiuchumi wilayani humo, hususan katika sekta ya utalii. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha halmashauri inanufaika ipasavyo kupitia tozo za huduma na vyanzo vingine vya mapato kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.


Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ngorongoro, Hamza Hussein Hamza, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro katika mkutano huo, aliwataka madiwani kuendelea kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao ili kuongeza mapato ya halmashauri na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.


Aidha, aliwasisitiza madiwani kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika kutatua changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi. Alisema ushirikiano huo utasaidia kuimarisha utendaji kazi wa serikali na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro.

HALMASHAURI YA WILAYA YA NGORONGORO KUENDELEA KUUNGA MKONO MIRADI YA WANANCHI, YAUNDA KAMATI MAALUM YA MAPATO HALMASHAURI YA WILAYA YA NGORONGORO KUENDELEA KUUNGA MKONO MIRADI YA WANANCHI, YAUNDA KAMATI MAALUM YA MAPATO Reviewed by VISION MEDIATZBLOG on June 06, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.