Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge, Mheshimiwa Daniel Sillo, amewataka wananchi kuendelea kuipenda nchi yao, kulinda amani na kuwa wasikivu kwa viongozi, akisisitiza kuwa mshikamano na utulivu wa Taifa ni msingi wa maendeleo.
Sillo ametoa rai hiyo wakati wa shughuli maalum ya dua, sala na maombezi ya kuliombea Taifa, Rais, viongozi na wananchi wote iliyofanyika katika Kijiji cha Qameyu, Kata ya Qameyu, Wilaya ya Babati mkoani Manyara.
Akizungumza mbele ya mamia ya wananchi waliohudhuria, Sillo aliwataka Watanzania kupuuza watu wasiolitakia mema Taifa na kuepuka kufuata taarifa za upotoshaji zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii ambazo zinaweza kuhatarisha amani na umoja wa nchi.
Pia aliwasisitiza vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa njia yenye manufaa badala ya kueneza chuki dhidi ya viongozi au kuchochea migawanyiko inayoweza kuvuruga amani na utulivu wa Taifa.
Alisema vijana wanapaswa kuwa waadilifu na kutambua kuwa bila amani hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kuwaombea viongozi wa nchi ili wapate hekima katika kuwatumikia Watanzania.
Sillo alieleza kuwa Rais anaendelea kufanya kazi kubwa ya kuunganisha Taifa, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kushiriki katika kulinda umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.
Aidha, aliwataka viongozi wa dini kutokuchoka kuliombea Taifa, akisema maombi yana mchango mkubwa katika kudumisha amani, utulivu na maendeleo ya nchi.
Katika ibada hiyo, Askofu Mathew Jacob wa Kanisa la Disciple Nations Pentecost Church (DNPC) Mbulu, aliyekuwa akihubiri kwa mamia ya waumini na wananchi, alisisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka zilizopo kwa mujibu wa mafundisho ya dini, akieleza kuwa heshima kwa viongozi ni nguzo muhimu ya kudumisha amani na utulivu.
Shughuli hiyo iliwakutanisha viongozi wa dini mbalimbali pamoja na wazee wa kimila wa jamii ya Iraqw kutoka Kata ya Qameyu, ambapo mamia ya wananchi walishiriki kwa pamoja kuiombea Tanzania, viongozi wake na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
Naye Diwani wa Kata ya Qameyu, Bernard Fissoo, alisema upendo ndiyo msingi wa kila jambo, akiwahimiza wananchi kuendelea kuishi kwa umoja, kuheshimiana na kushirikiana katika kujenga jamii yenye amani na maendeleo.
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
July 04, 2026
Rating:



No comments: