BARAZA LA MADIWANI BABATI MJINI LAITAKA KAMISHENI YA ARDHI KUSHUGHULIKIA MAENEO YENYE NIGOGORO YA ARDHI
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara limeitaka Kamisheni ya Ardhi kuhamishia huduma zake karibu na maeneo yenye migogoro ya ardhi, likisema hatua hiyo itasaidia kudhibiti udanganyifu unaoigharimu halmashauri kwa malipo makubwa ya fidia katika maeneo yaliyopatikana kwa gharama ndogo.
Agizo hilo limetolewa leo katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo mwaka, ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Yonna Wawo, amesema baadhi ya migogoro ya ardhi imekuwa ikiisababishia halmashauri hasara kubwa kutokana na madai ya fidia yanayoongezeka katika maeneo ya taasisi na miradi ya umma.
Amesema uwepo wa ofisi za Kamisheni ya Ardhi karibu na maeneo yenye migogoro utarahisisha utatuzi wa malalamiko kwa wakati na kupunguza mianya ya udanganyifu ambayo imekuwa ikiathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Afisa wa Kamisheni ya Ardhi, Amon Nzalalila, amesema baadhi ya migogoro hiyo husababishwa na wananchi kurejea na madai yale yale kila panapobadilika viongozi au mamlaka za maamuzi, jambo linalochelewesha utatuzi wa migogoro na kuongeza malalamiko.
Naye baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Babati wamekiri kuwepo kwa changamoto ya migogoro ya ardhi, wakisema imekuwa ikisababisha migongano ya mara kwa mara kati ya wananchi na taasisi mbalimbali pamoja na kuchelewesha utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo.
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
August 04, 2026
Rating:

No comments: