test

WATU WAWILI WALIWA NA FISI BABATI

 Wakazi wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara wameingiwa na hofu baada ya watu wawili kupoteza maisha katika mashambulizi mawili tofauti yanayodaiwa kufanywa na fisi usiku wa kuamkia Jumatano, Agosti 5, 2026, huku viongozi wa maeneo hayo wakitoa wito kwa mamlaka za wanyamapori kuchukua hatua za haraka kukabiliana na tishio hilo.



Katika tukio la kwanza lililotokea Kijiji cha Gidingwar, mwanaume aliyefahamika kwa jina la Antony Saqwere, anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35 na ambaye alikuwa mwalimu wa kwaya wa Kanisa Katoliki kutoka Kijiji cha Donya, alidaiwa kuliwa na fisi hadi kubaki sehemu ndogo tu za mwili wake.


Mwenyekiti wa Kijiji cha Gidingwar, Paulo Afirkanus, amesema walipofika eneo la tukio walikuta nguo za marehemu, damu, baadhi ya mifupa pamoja na fuvu la kichwa pekee.


Amesema polisi walifika eneo hilo na kukusanya mabaki hayo kwa ajili ya uchunguzi na taratibu nyingine.


Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, majirani walieleza kuwa walisikia mafisi wengi wakibweka usiku kucha, hali inayoashiria kuwa huenda kundi la fisi lilihusika na tukio hilo.


Wakati huo huo, tukio jingine limetokea katika eneo la Dareda Mission, ambapo mwanaume aliyefahamika kwa jina la Manase Nicodemus, mwenye umri wa zaidi ya miaka 40, alifariki dunia baada ya kushambuliwa na fisi.


Diwani wa Kata ya Dareda, Willbrod John Bayo, amesema marehemu alikuwa akifahamika na wakazi wa eneo hilo na inasadikiwa alikuwa amelewa kupita kiasi kabla ya kushambuliwa na fisi.


Amesema kutokana na hali ya mwili wake, inaaminika alishambuliwa na fisi mmoja kwani sehemu zilizoliwa ni miguu na tumbo, huku sehemu nyingine za mwili zikibaki salama.


Diwani huyo amesema tukio hilo limetokea karibu na nyumba za mapadri eneo la Dareda Mission na mwili wa marehemu ulikutwa na wananchi majira ya asubuhi.


Aidha, amesema tayari amewasiliana na mamlaka husika za wanyamapori kuhusu ongezeko la fisi wanaoingia kwenye makazi ya wananchi usiku kutafuta chakula, akieleza kuwa hali hiyo imeendelea kuwa tishio kwa usalama wa wananchi.


Matukio hayo yanakuja ikiwa ni siku chache tangu kuripotiwa mashambulizi mengine ya fisi katika eneo la Masakta Mkoa wa Manyara, jambo linaloibua wasiwasi kuhusu ongezeko la wanyama hao karibu na makazi ya watu na kuimarisha wito wa wananchi kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuondoa tishio hilo.

WATU WAWILI WALIWA NA FISI BABATI WATU WAWILI WALIWA NA FISI BABATI Reviewed by VISION MEDIATZBLOG on August 05, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.