test

EASTRIP YAACHA ALAMA DIT, UDAHILI WA WANAFUNZI WAONGEZEKA HUKU MAFUNZO YA VITENDO YAKIIMARIKA

  Na Mwandishi Wetu.

Mradi wa EASTRIP umechangia kuimarisha elimu ya ufundi nchini Tanzania kupitia uboreshaji wa miundombinu, vifaa vya kujifunzia na uwezo wa wakufunzi, huku ukisaidia kuandaa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika sekta mbalimbali za uchumi.

Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Frederick Salukele, amesema hayo leo, Oktoba 26, 2026, katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana na Benki ya Dunia ambao ndio wafadhili wa mradi. 

Salukele amebainisha mafanikio ya mradi huo  unaotekelezwa katika vituo vinne vya umahiri ambavyo ni DIT Dar es Salaam, DIT Mwanza, Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Ufundi Arusha, ambapo DIT Kampasi ya  Dar es Salaam, inayojikita katika teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), imezalisha wataalamu wanaofanya kazi katika sekta za viwanda, benki na madini, wakati DIT Mwanza imeanzisha kiwanda na kuzalisha wataalamu katika sekta ya kuchakata ngozi na kutengeneza bidhaa kama viatu, pochi, mabegi, mikanda na makoti.

Kwa upande wa NIT, amesema mradi unawezesha kuandaa eneo la mafunzo kwa wataalamu wa injini za ndege, huku wataalamu wa chuo hicho wakishiriki nje ya nchi katika majaribio ya kiwandani (Factory Acceptance Test) ya ndege inayotarajiwa kuletwa Tanzania.

Ameongeza kuwa Chuo cha Ufundi Arusha kinaendelea na mradi wa mtambo wa kuzalisha umeme wenye uwezo wa megawati 1.65, ambao umefikia hatua za kuunganisha umeme kwenye gridi ya taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa DIT, Profesa Preksedis Marco Ndomba, amesema EASTRIP imewezesha upatikanaji wa maabara za kisasa za TEHAMA, usalama wa mifumo ya kompyuta (*Cybersecurity*), roboti na akili unde (AI), pamoja na vifaa vya kujifunzia na mafunzo kwa wakufunzi.

Amesema mradi huo pia umefungua fursa za ushirikiano wa kitaaluma na vyuo vya nje kupitia programu za shahada  na chuo kikuu cha Chongqing nchini China na Chuo cha Rudn nchini Urusi kwenye masuala ya Teknolojia ya anga za mbali. (Space Technology) 

Aidha, ameishukuru Serikali kwa kufadhili kiwanda chenye thamani ya Sh bilioni 7 katika kampasi ya DIT Mwanza, kitakachowezesha wanafunzi kujifunza kwa vitendo katika mazingira ya uzalishaji viwandani.

Profesa Ndomba amesema mafanikio ya mradi huo yanaonekana pia katika ongezeko la udahili wa wanafunzi DIT, kutoka 3,000 miaka 10 iliyopita hadi 14,000 mwaka 2026.

Mradi wa EASTRIP ulianza mwaka 2019 na unatekelezwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Ethiopia kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Awali ulipangwa kukamilika mwaka 2024, lakini muda wake umeongezwa hadi Desemba 2026 ili kukamilisha shughuli zilizobaki.





.










EASTRIP YAACHA ALAMA DIT, UDAHILI WA WANAFUNZI WAONGEZEKA HUKU MAFUNZO YA VITENDO YAKIIMARIKA EASTRIP YAACHA ALAMA DIT, UDAHILI WA WANAFUNZI WAONGEZEKA  HUKU MAFUNZO YA VITENDO YAKIIMARIKA Reviewed by Adery Masta on October 26, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.