test

WANANCHI WA KITONGOJI CHA SABURI MAKUYUNI WAOMBA MSAADA WA HARAKA SERIKALINI DHIDI YA MWEKEZAJI

 

Wananchi wa Kijiji cha Makuyuni, Kitongoji cha Saburi kilichopo Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha, wametoa taarifa ya dharura na kuomba ulinzi na uingiliaji kati wa haraka kutoka kwa viongozi wa Serikali dhidi ya vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na mwekezaji anayeitwa Akram Aziz.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Oktoba 3, 2026, wananchi hao wamesema mwekezaji huyo amefika kwenye kitongoji chao akiwa na tingatinga kubwa (bulldozer) kwa lengo la kubomoa nyumba zaidi ya 600, pamoja na kuharibu misikiti, kanisa, shule na zahanati.



Wamesema kitendo hicho kimesababisha taharuki kubwa na kuzuka kwa vurugu kati ya vibaraka wa mwekezaji huyo na wananchi waliokuwa wakitetea haki na mali zao, jambo lililomlazimu mwekezaji kukimbia ili kunusuru maisha yake kutokana na ghadhabu za wananchi.


Wananchi hao wameeleza kuwa wameishi katika Kitongoji cha Saburi kwa zaidi ya miaka 30, ambapo eneo hilo walipewa kihalali na mwekezaji aliyetangulia, na baadaye Halmashauri ilipima na kuweka alama (beacons) kutenga eneo hilo kutoka katika shamba la mwekezaji.


Ameelezwa kuwa eneo hilo kwa sasa limetambuliwa na kusajiliwa rasmi na TAMISEMI kama Kitongoji kinachojitegemea, chenye miundombinu kamili ikiwemo shule, zahanati, misikiti na kanisa, pamoja na miundombinu ya umeme wa REA na visima vya maji.


Aidha, wananchi hao wamesema mwaka 2025 Halmashauri ilimuandikia barua rasmi mwekezaji huyo ikimtaka aachie ekari 400 ili kupisha makazi ya wananchi hao, hata hivyo mwekezaji huyo amegoma kutii agizo hilo.


Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wameiomba Serikali kupitia Ofisi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za dharura ikiwemo kumzuia mara moja mwekezaji huyo kufanya jaribio lolote la kubomoa makazi na taasisi za kijamii katika Kitongoji cha Saburi, kufanya uchunguzi wa dharura kuhusu hati anazozitumia kujitwalia ardhi ya wananchi, pamoja na kulinda usalama wa maisha na mali zao kwa kupeleka vyombo vya ulinzi.


"Haiwezekani wananchi wa Kitongoji cha Saburi tuwe wakimbizi ndani ya nchi yetu wenyewe baada ya kuishi kwa zaidi ya miaka 30. Tunaomba msaada wa haraka," wamesema wananchi hao.

WANANCHI WA KITONGOJI CHA SABURI MAKUYUNI WAOMBA MSAADA WA HARAKA SERIKALINI DHIDI YA MWEKEZAJI WANANCHI WA KITONGOJI CHA SABURI MAKUYUNI WAOMBA MSAADA WA HARAKA SERIKALINI DHIDI YA MWEKEZAJI Reviewed by VISION MEDIATZBLOG on October 23, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.