test

Mabomu Baridi yaanza kutumika Doria za Tembo



Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii  kwa ubunifu  wa  kuvumbua bomu baridi lililoboreshwa kwa ajili ya kupambana wanyama hatari kama Tembo kwa kushirikiana na  Shirika la Mzinga.



Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava wakati wa hafla  maalum ya Wizara  ya Maliasili na Utalii  ya kupokea mabomu 4000 yaliyotengenezwa  na Shirika la Mzinga mjini Morogoro.



Mara baada ya kupokea mabomu hayo  Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza operesheni maalum katika Halmashauri 20 nchini na inaongozwa na  Naibu Katibu Mkuu CP  Benedict Wakulyamba. 



"Naomba kutoa  pongezi za dhati kwa Wizara na Shirika kwa kuja na suluhisho hili na natoa wito kwa halmashauri zinazosumbuliwa na Tembo kununua na kutumia mabomu haya ili kupambana na wanyama hao." amesisitiza  Mhe. Mnzava.



Ameitaka Wizara kuendelea  kutoa mafunzo kwa askari wa vijiji na vijana  kwa kuwa Serikali peke yake haitaweza.


"Hii ni kazi ya sisi sote, Serikali peke yake haitaweza ni lazima kuendelea   kuwashirikisha wananchi kwa kuwapa elimu" ameongeza.


 Pia ameiomba Wizara kuendelea kufanya tafiti ili kubuni mbinu nzuri zaidi za kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuzingatia kuwa Tembo wamekuwa wakizoea mbinu na kuendelea kuleta usumbufu.


Mwakilishi wa wabunge kutoka kwenye majimbo yenye changamoto za Tembo walioshiriki hafla hiyo,  Mhe. Salma Kikwete  amempongeza  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wizara kwa kuendelea kutatua changamoto hiyo.


"Leo klla Mbunge amefurahi kwa kuwa hili ni jambo kubwa ambalo litaleta suluhisho na sasa  tunakwenda kurudisha salamu kwa wananchi wetu kazi hii nzuri iliyofanywa na wananchi" amesisitiza huku  akitaka elimu iendelee kutolewa.


Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesema wizara yake itaendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo ya viongozi wakuu na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii.



Aidha, amesema uvumbuzi wa  bomu hilo baridi ni utekelezaji wa maelekezo ya  Rais Samia aliyoitaka  wizara kuja na ufumbuzi wa changamoto hiyo.


Ameeleza kuwa wizara yake itaendelea kuja na ubunifu mbalimbali kwa kuwa hakuna njia moja pekee ya kukabiliana na changamoto hiyo.


Ametumia jukwaa hilo pia kutoa pole kwa wananchi wote ambao  wameathirika kwa namna moja au nyingine.


Hafla hiyo pia iliwashirikisha  wabunge, Naibu Katibu Mkuu C.P  Benedict Wakulyamba, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Ulinzi na  menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mabomu Baridi yaanza kutumika Doria za Tembo Mabomu Baridi yaanza kutumika Doria za Tembo Reviewed by VISION MEDIATZBLOG on May 23, 2024 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.