Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda Mei 9, 2024 amekutana na Wakuu wa Taasisi za Umma, viongozi wa Wamachinga na viongozi wa Wafanyabiashara kwa lengo la kufahamiana na kufahamu shughuli zao.
Mhe. Mtanda amekutana na viongozi hao kwa nyakati tofauti katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkuu wa Mkoa ambapo amewasisitiza viongozi wa taasisi kutambua wajibu wao kwa kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi wanaowahudumia.
"Rais Samia ameonesha kwa vitendo anavyopigania maendeleo ya wananchi na sisi tunavyotoa huduma bora wananchi watazidi kuifurahia Serikali yao," amesisitiza Mhe. Mtanda.
Amewataka viongozi hao kutekeleza wajibu wao kwa kuimarisha nidhamu ya utumishi wa umma kwa kufanya kazi kwa upendo, kuheshimiana na kuepuka aina yoyote ya unyanyasaji au kupokea rushwa kutoka kwa wananchi.
Vilevile aliwataka viongozi kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano na kuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa kwa wananchi pindi kutokeapo tatizo lolote.
“Wananchi wanapaswa kupewa taarifa sahihi na kwa wakati endapo kuna dharura ya huduma; taasisi inapaswa kutoa taarifa kwa wakati kwa wananchi ili mwananchi ajue kinachoendelea na siyo kukaa kimya,” amesema Mhe. Mtanda.
Amesema yupo mbioni kuanza ziara kutembelea maeneo yote mkoani humo ili kujionea maendeleo ya wananchi na changamoto zinazowakabili.
"Ndugu viongozi mkutano huu sio wa kusikiliza changamoto zenu na kuzitolea majibu hapa la hasha! lengo ni kufahamiana na kujua shughuli zenu mkitambua sina muda mrefu tangu nihamishiwe hapa nikitokea Mara," amesema Mhe. Mtanda.
Akimalizia mkutano huo na viongozi, Mkuu huyo wa Mkoa amebainisha kuwa anatambua mchango wao katika pato la Taifa na kusisitiza kuendelea kushirikiana katika ujenzi wa Taifa.
No comments: