Kaimu Mkurugenzi wa Yas – Kanda ya Kaskazini, Bw. Daniel Mainoya (wa pili kushoto), akimkabidhi zawadi Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude (wa pili kulia), wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa chapa za Yas na Mixx by Yas mkoani Arusha. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano – Mixx by Yas, Justine Lawena, na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa – Yas Business, Anatory Lelo.
Na Mwandishi Wetu.
Arusha, Tanzania – Kampuni ya mawasiliano ya YAS imewataka wafanyabiashara na wananchi mkoani Arusha kuchangamkia fursa za kujikwamua kiuchumi kupitia teknolojia na huduma jumuishi za kifedha zinazotolewa na kampuni hiyo. Huduma hizo zinajumuisha mikopo, uwakala, pamoja na malipo ya serikali kwa gharama nafuu, zikiwa na lengo la kurahisisha maisha ya wananchi wa mijini na vijijini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa chapa ya YAS na Mix by YAS uliofanyika mkoani Arusha, Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini wa kampuni ya YAS, Daniel Mainoya, alisema kuwa YAS inaleta mapinduzi ya huduma za kifedha kidigitali, hususan kwa vijana, ili kuboresha maisha yao na kuongeza fursa za kiuchumi.
"Yas ni mwelekeo mpya wa kidijitali. Ni chapa inayolenga kuwezesha vijana, wafanyabiashara wadogo na wa kati, na kila Mtanzania anayetafuta fursa za kujikwamua kupitia teknolojia na huduma bora za kifedha. Kupitia Yas, tunajenga jamii inayoweza kufanikisha ndoto zake kupitia suluhisho rahisi, nafuu, na za kisasa.
Kupitia Yas na Mixx by Yas, tunasimamia falsafa ya PACE – Personal, Accessible, Consistent, and Effortless, ambayo inaakisi dhamira yetu ya kutoa huduma bora, zinazobadilisha maisha, na kuleta thamani halisi kwa wateja wetu."
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, aliipongeza YAS kwa ubunifu na mchango wake katika kuinua uchumi wa wananchi kupitia huduma bora. Alitoa wito kwa wakazi wa Arusha kutumia kikamilifu huduma hizo ambazo zimebuniwa kujibu mahitaji ya wananchi wa maeneo ya mijini na vijijini.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa wa YAS, Antony Lelo, alibainisha kuwa kampuni hiyo inatoa mikopo ya hadi shilingi milioni mbili kwa wateja pamoja na huduma mbalimbali za malipo, hasa kwa makundi kama wakulima, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali.
Kwa ujumla, YAS imejikita katika kuhakikisha kuwa huduma zake zinapatikana kwa urahisi, usalama na kwa gharama nafuu, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono ajenda ya taifa ya kujumuisha wananchi wote katika huduma za kifedha.
