test

TBS WAWAFIKIA WAJASIRIAMALI WANAOZALISHA NISHATI SAFI YA MKAA MBADALA - KIGOMA

 Na Mwandishi Wetu.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa mafunzo maalum kwa wajasiriamali wanaojihusisha na uzalishaji wa nishati safi ya mkaa mbadala katika mkoa wa Kigoma, ikiwa ni hatua muhimu katika kukuza sekta ya nishati rafiki kwa mazingira na kuimarisha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wazalishaji hao ili waweze kuzalisha mkaa mbadala unaokidhi matakwa ya viwango vya ubora vilivyowekwa. Kupitia mafunzo hayo, wajasiriamali wamepata uelewa mpana kuhusu mbinu bora za uzalishaji, udhibiti wa ubora pamoja na namna ya kuongeza thamani ya bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko la ndani na hata soko la kimataifa.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa Viwango wa TBS, Spiradson Kagaba, aliwahimiza wajasiriamali kuzingatia viwango vilivyowekwa ili kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakuwa salama kwa watumiaji na pia zinachangia kulinda mazingira. Alisisitiza kuwa uzalishaji unaozingatia viwango huongeza uaminifu wa bidhaa sokoni na kuwapa wazalishaji fursa kubwa zaidi za biashara.

Aidha, TBS imeeleza kuwa matumizi ya mkaa mbadala yana manufaa makubwa kwa jamii na mazingira. Mbali na kusaidia kupunguza taka zinazoweza kutumika kama malighafi ya uzalishaji, mkaa mbadala hutoa moshi mdogo unaoweza kuathiri afya za binadamu, huwaka kwa muda mrefu zaidi na hivyo kuwa na ufanisi mkubwa katika matumizi ya nishati majumbani na kwenye biashara ndogo ndogo.

Hatua hii pia inaendana na mkakati wa Serikali wa kupunguza ukataji holela wa miti unaochangiwa na matumizi makubwa ya mkaa wa kawaida. Kupitia uhamasishaji wa matumizi ya nishati mbadala, Serikali inalenga kulinda uoto wa asili na kuimarisha juhudi za kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mafunzo haya yanaashiria dhamira ya TBS ya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinazingatia viwango vinavyotambulika, huku zikichochea maendeleo ya uchumi wa wajasiriamali na taifa kwa ujumla.






TBS WAWAFIKIA WAJASIRIAMALI WANAOZALISHA NISHATI SAFI YA MKAA MBADALA - KIGOMA TBS WAWAFIKIA WAJASIRIAMALI WANAOZALISHA NISHATI SAFI  YA MKAA MBADALA - KIGOMA Reviewed by Adery Masta on March 16, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.