Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, leo Aprili 30, 2026, limeketi na kujadili masuala mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026.
Akihutubia baraza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Mhe. Michael Semindu, amelitaka baraza kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato, akisisitiza kuwa mapato ya ndani ndiyo msingi wa maendeleo ya halmashauri.
Mhe. Semindu aliwahimiza madiwani na wataalamu kuwa wabunifu katika kubuni na kuibua vyanzo vipya vya mapato, sambamba na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji ili kuongeza ufanisi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, Mhe. Dkt. Emanuel Nuwas, amesema kuwa kupitia ushirikiano kati yake na baraza, imewezekana Shule ya Sekondari Bishop Hhando kuanzisha masomo ya kidato cha tano na sita.
Aidha, Mhe. Dkt. Nuwas aliwataka Waheshimiwa Madiwani kuorodhesha vitongoji ambavyo havina umeme ili viweze kuingizwa katika mipango ya usambazaji wa umeme, akibainisha kuwa katika awamu ya kwanza, vitongoji 59 vitapatiwa huduma hiyo.
Vilevile, alimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa kupeleka wataalamu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) katika kata mbalimbali, hatua iliyosaidia kuongeza idadi ya wananchi wanaopata vitambulisho.
Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Mhe. Yeconia Delles, aliwapongeza wataalamu wa elimu kwa matokeo mazuri ya wanafunzi wa darasa la saba na kidato cha nne, akihimiza juhudi zaidi ziendelee kudumishwa ili kuongeza ufaulu.
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
April 30, 2026
Rating:






No comments: