test

ULEVI WAWAPONZA MADEREVA 6 MWANZA, WAFUNGIWA LESENI

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewakamata madereva sita wa magari kwa kosa la kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa pombe, huku leseni zao zikifungiwa kwa muda wa miezi sita.


Akizungumza leo Jumamosi Aprili 4, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, amesema hatua hiyo ni sehemu ya operesheni maalum inayoendelea ya kudhibiti ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Amesema madereva hao walikamatwa Aprili 3, 2026 wakiendesha magari yao wakiwa katika hali ya ulevi, na kwamba watachukuliwa hatua zaidi za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.



Madereva waliokamatwa ni Suleiman Magoti (36), mkazi wa Nyakato, aliyekuwa akiendesha Toyota Hiace) kati ya Kakebe na Uwanja wa Ndege; Elias Michael (28), mkazi wa Nyegezi, dereva wa Toyota Coaster kati ya Kisesa na Usagara; na Ramadhani Athuman (56), aliyekuwa akiendesha Toyota Hiace kati ya Uwanja wa Ndege na Nyashishi.

Wengine ni Joeli Ezekiel (36), mkazi wa Nyakato Mecco, aliyekuwa akiendesha Toyota Town Ace Pickup Fidelis Rong’ongo (27), mkazi wa Musoma, dereva wa Toyota Crown pamoja na Shaban Siraji (55), mkazi wa Capripoint, aliyekuwa akiendesha Toyota Hiace kati ya Ilemela na Nyashishi.

Katika operesheni hiyo, Polisi pia wamekamata jumla ya pikipiki za magurudumu matatu 98 na pikipiki tano za magurudumu mawili zilizobainika kuwa na mabadiliko yasiyoruhusiwa ikiwemo kukatwa kwa mifumo ya kutolea moshi (muffler). Aidha, magari 13 ya abiria na manne madogo yalikamatwa kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani, ikiwemo ulevi na kuendesha bila leseni.

DCP Mutafungwa ametoa wito kwa madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kuepusha ajali.

“Ni muhimu kuondoa taa zisizoruhusiwa, kuhakikisha vyombo vina namba halali za usajili pamoja na kuwa na leseni stahiki,” amesema.

Aidha, amesisitiza kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja, akiwataka watumiaji wa barabara kushirikiana katika kulinda maisha na mali za wananchi.


ULEVI WAWAPONZA MADEREVA 6 MWANZA, WAFUNGIWA LESENI ULEVI WAWAPONZA MADEREVA 6 MWANZA, WAFUNGIWA LESENI Reviewed by VISION MEDIATZBLOG on April 04, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.