test

KITUO CHA AFYA CHA ZAIDI YA MILIONI 400 CHAFUNGULIWA KATA YA MARETADU

 


Wananchi wa Kata ya Maretadu, Wilaya ya Mbulu, wanatarajiwa kunufaika na huduma bora za afya kufuatia ufunguzi wa Kituo cha Afya cha Maretadu kilichogharimu zaidi ya shilingi milioni 400 kujengwa.




KITUO hicho Cha Afya kilichofunguliwa  Mei 28, 2026 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbulu, Ndugu Paulo Bura, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Mheshimiwa Michael Semindu kimegharimu  shilingi milioni 442.5, ambapo Serikali Kuu imetoa shilingi milioni 400, Halmashauri ikachangia shilingi milioni 30 kupitia mapato ya ndani, huku wananchi wakichangia shilingi milioni 12.5.




Kituo hicho ambacho kimefunguliwa kwa kuanza kutoa huduma za wagonjwa wa nje  (OPD) kinatarajiwa  kuhudumia zaidi ya wananchi elfu 15 kutoka ndani na nje ya Kata ya Maretadu.


Akifungua jengo hilo la OPD, Ndugu  Bura aliwapongeza wananchi wa Maretadu kwa ushiriki wao mkubwa katika utekelezaji wa mradi huo. Pia aliwataka kuendelea kutunza miundombinu hiyo kutokana na gharama kubwa zilizotumika kujenga kituo hicho.


Sambamba na hilo, aliwataka watumishi wa afya na wauguzi kutoa huduma kwa lugha nzuri na upendo ili kituo hicho kiwe faraja kwa wananchi badala ya kuwa chanzo cha malalamiko.


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Mheshimiwa Yeconia Delles, aliwapongeza wananchi wa Maretadu kwa ushirikiano wao katika ujenzi wa kituo hicho na kuwasisitiza kuendelea kushirikiana na Serikali ili kukamilisha majengo yaliyosalia kwa ajili ya kuboresha zaidi huduma za afya.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Ndugu Abubakar Kuuli, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za kuboresha sekta ya afya wilayani hapa.


 Alisema kuwa kuanzia mwaka 2021 hadi 2026, jumla ya vituo vya afya vitano vimeongezeka wilayani Mbulu.


Nae Mbunge wa Mbulu Vijijini, Mheshimiwa Dkt. Emanuel Nuwas, aliwapongeza wananchi na viongozi wote waliofanikisha ujenzi wa kituo hicho, akieleza kuwa wananchi walikuwa wakipata changamoto kubwa kufuata huduma za afya katika kata za Haydom na Dongobesh ambazo zipo mbali.


KITUO CHA AFYA CHA ZAIDI YA MILIONI 400 CHAFUNGULIWA KATA YA MARETADU KITUO CHA AFYA CHA ZAIDI YA MILIONI 400 CHAFUNGULIWA KATA YA MARETADU Reviewed by VISION MEDIATZBLOG on May 28, 2026 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.