Mwenyekiti wa Mtaa wa Hangoni, Hamidu Ramadhani, amesema mtuhumiwa anayehusishwa na mauaji ya mwanamke aitwaye Joyce Antony Amo (33), mkazi wa Mtaa wa Hangoni mjini Babati mkoani Manyara, alifunga mlango wa nyumba kwa nje mara baada ya kutekeleza tukio hilo na kutoweka kusikojulikana.
Hadi sasa, mtuhumiwa huyo hajapatikana.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Hamidu amesema mwanamke huyo hakuonekana kazini siku ya tukio, jambo lililozua wasiwasi kwa wenzake.
Baadaye watoto wake waliporudi kutoka shuleni walikuta mlango wa nyumba umefungwa kwa nje, ndipo wakaelekea mahali alipokuwa akifanya kazi kuulizia taarifa zake.
"Walijibiwa kuwa siku hiyo mama yao hakuwa ameonekana kabisa kazini.
Wakaambatana na baadhi ya watu kurejea nyumbani, ambapo walipochungulia dirishani waliona hali isiyo ya kawaida.
Vyombo vilikuwa vimevurugwa na damu zimetapakaa ndani ya nyumba," amesema Mwenyekiti huyo.
Ameongeza kuwa baada ya mlango kuvunjwa, walimkuta Joyce tayari akiwa amefariki dunia, akiwa amekatwa shingoni kwa kitu chenye ncha kali na mwili wake ukiwa umeviringishwa kwenye shuka.
Mwenyekiti huyo amesema baada ya kubaini tukio hilo, alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, ambalo lilifika haraka katika eneo la tukio na kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kabla ya kuuchukua na kuupeleka hospitalini kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti, marehemu Joyce Antony Amo aliuawa Julai 24, 2026.
Inaelezwa kuwa yeye na mtuhumiwa walikuwa wanandoa, lakini walikuwa wametengana kwa muda na kila mmoja kuishi kivyake kufuatia kutofautiana.
Familia imesema maziko ya marehemu yanatarajiwa kufanyika Jumanne, Julai 28, 2026, katika kijiji cha Mamaisara, wilayani Mbulu, mkoani Manyara
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
July 27, 2026
Rating:

No comments: