Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Hashim Mgandilwa, wameshiriki mazishi ya Elia Paul Masong', mtoto wa Diwani wa Kata ya Arri, aliyefariki Novemba 21, 2026 baada ya kupata ajali ya pikipiki.
Elia Paul amefariki akiwa na miaka 17, huku akiwa anatarajiwa kuanza Kidato cha Nne mwaka 2027.
Katika mazishi hayo, viongozi hao wameweka shada la maua kwenye kaburi la marehemu kama ishara ya heshima, upendo na kumuaga kwa mara ya mwisho.
Akizungumza katika mazishi hayo, Mhe. Mgandilwa amewataka wananchi kuishi hapa duniani wakiwa wamejiandaa, kwani hakuna anayejua muda wala siku ya kuondoka hapa duniani.
Amesema kifo hakijali cheo, nafasi, wala uchumi. Mtu anaweza kuwa na cheo kikubwa, awe na mali nyingi, au awe na nafasi kubwa katika jamii, lakini siku ya kuondoka ikifika, vyote hivyo vinabaki duniani.
Ndiyo maana amewataka watu wote kuishi kwa unyenyekevu, upendo, na kumcha Mungu, huku wakiwa wamejitayarisha kila siku, kwani kifo hakibagui.
Mhe. Mgandilwa amewafariji wafiwa na kuwaombea subira katika kipindi hiki kigumu, huku akiwataka wananchi kuendelea kumuombea marehemu apumzike kwa amani.
Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi.
Amen..
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
November 23, 2026
Rating:




No comments: