test

KAMPUNI YA YAS KUWAWEZESHA WATOTO WA KIKE KATIKA TEHAMA

 Na Mwandishi Wetu.

Katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuhimiza wasichana kusoma masomo ya sayansi, taasisi ya Apps and Girls ya jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Yas Tanzania imeendesha programu maalum ya mafunzo kwa wanafunzi wa sekondari kutoka shule tisa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Desemba 13, 2024, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Carolyne Ekyarisiima, alisema mpango huo unalenga kuondoa tofauti ya kijinsia katika masomo ya sayansi na kuwajengea wasichana uwezo wa kujiajiri.

"Tunatoa mafunzo haya kuanzia ngazi ya shule za sekondari hadi kwa wale walio nje ya mfumo rasmi wa elimu. Wanajifunza kutengeneza roboti, kuelewa akili bandia, na kupata ujuzi wa ujasiriamali," alisema Carolyne.

Aliongeza kuwa programu hiyo pia ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono sera ya serikali ya kuongeza ushiriki wa wasichana katika masomo ya sayansi.

"Kila baada ya programu, wanafunzi hushindana kuunda miradi ya kiteknolojia, ambapo washindi hupewa zawadi ili kuwahamasisha zaidi," alibainisha.

Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano ya Nje wa Yas Tanzania, Rukia Mtingwa, alisema taasisi yao imeungana na Apps and Girls kusaidia kuhamasisha wasichana kuchukua masomo ya sayansi kutokana na uwiano mdogo wa kijinsia katika nyanja hiyo.

"Tunatoa mchango wetu kwa kuwapa vijana wetu mafunzo ya TEHAMA ambayo yatawasaidia darasani na hata baada ya kumaliza masomo yao," alisema Rukia.

Mmoja wa wanafunzi waliopokea mafunzo hayo, Maria Mtega, alisema kuwa programu hiyo imewajengea kujiamini na kutambua uwezo wao katika masomo ya sayansi na teknolojia.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuleta mapinduzi chanya kwa kuongeza ushiriki wa wasichana katika sekta za sayansi na teknolojia nchini Tanzania.

KAMPUNI YA YAS KUWAWEZESHA WATOTO WA KIKE KATIKA TEHAMA KAMPUNI YA YAS KUWAWEZESHA WATOTO WA KIKE KATIKA TEHAMA Reviewed by Adery Masta on December 15, 2024 Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.