Chuo cha Polisi Wanamaji Mkoa wa Mwanza kimepokea boti moja ya kisasa aina ya Fiber Speed Boat PB 23 PAPA, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha mafunzo kwa vitendo, doria za majini na usalama ndani ya Ziwa Victoria.
Boti hiyo ilikabidhiwa rasmi tarehe 2 Februari, 2026, baada ya kubadilishiwa matumizi kutoka Makao Makuu ya Kikosi cha Polisi Wanamaji Dar es Salaam, kufuatia uamuzi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi wa kusogeza vitendea kazi karibu na maeneo ya utekelezaji wa majukumu.
Akikabidhi boti hiyo kwa Mkuu wa Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza, SACP Ndagile Makubi, Mkuu wa Kikosi cha Polisi Wanamaji Tanzania, SACP Moshi Sokoro, alisema uhamisho wa boti hiyo unalenga kuongeza ufanisi wa mafunzo kwa wanafunzi wanaopata mafunzo chuoni hapo, hususan mafunzo ya uokoaji majini, doria, na operesheni maalum.
SACP Sokoro alibainisha kuwa kwa muda mrefu chuo na kikosi cha Polisi Wanamaji vilikabiliwa na changamoto ya uhaba wa vitendea kazi vya kufundishia kwa vitendo, hali iliyowalazimu kuazima boti kutoka kwa wadau mbalimbali, jambo lililokwamisha utekelezaji kamili wa majukumu. Alisema kuwasili kwa boti hiyo kutatatua changamoto hiyo na kuongeza ufanisi wa kazi za kila siku.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, ambaye alisema Mkuu wa Jeshi la Polisi ametoa boti hiyo kama sehemu ya mkakati wa kusogeza huduma za usalama kwa jamii, hususan kwa wakazi wa maeneo ya Ziwa Victoria. DCP Mutafungwa alisisitiza umuhimu wa kutunza boti na vifaa vingine vya Jeshi la Polisi, huku akiwataka wanafunzi wa chuo hicho kujifunza kwa bidii na kwa vitendo bila woga, hasa katika mafunzo ya ziwani.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, boti hiyo itatumika katika mafunzo ya kila siku ya askari, doria za majini, operesheni maalum, na shughuli za uokoaji, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi katika mialo, visiwani na maeneo yasiyofikika kirahisi. Hatua hiyo itasaidia Jeshi la Polisi kuwafikia wananchi kwa haraka, kudhibiti uhalifu wa majini na kukabiliana na matukio ya dharura kwa ufanisi zaidi.
Fiber Speed Boat PB 23 PAPA ina uwezo wa kubeba watu 15 kwa wakati mmoja, ikiwa na mwendo wa kasi na uwezo mkubwa wa kufika maeneo mbalimbali ndani ya Ziwa Victoria. Uwezo huo unatarajiwa kuimarisha doria, kuongeza ufanisi wa uokoaji, na kuboresha utekelezaji wa operesheni maalum ikilinganishwa na vifaa vilivyokuwepo awali.
Akizungumza mara baada ya kupokea boti hiyo, Mkuu wa Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza, SACP Ndagile Makubi, alitoa shukrani za dhati kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa kukipatia chuo hicho kifaa hicho muhimu. Alisema boti hiyo itaongeza kwa kiasi kikubwa ubora wa mafunzo ya uokoaji majini, kuimarisha doria, na kusaidia kudhibiti na kuzuia uhalifu ndani ya Ziwa Victoria.
Uboreshaji huu wa vitendea kazi ni dhamira ya dhati ya Serikali katika kuimarisha usalama wa wananchi na kuwekeza katika miundombinu ya ulinzi wa majini. Hatua hiyo inaendelea kukipa Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza hadhi ya kuwa kitovu muhimu cha mafunzo bora ya kitaifa, kikitoa mafunzo kwa askari wa Jeshi la Polisi, vyombo vingine vya usalama, watu binafsi pamoja na taasisi zisizo za kiserikali, sambamba na kuimarisha ulinzi thabiti na endelevu wa majini nchini.
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
February 06, 2026
Rating:





No comments: