“
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi kuwa tayari kumaliza migogoro ya ardhi katika maeneo yao huku akisisitiza kuwa suluhisho la migogoro mingi linaanzia kwa wananchi wenyewe kuwa na nia ya kuimaliza migogoro.
Mhe. Mtanda amesema hayo leo Mei 19, 2026 alipokuwa katika ziara ya kusikiliza na kutatua malalamiko pamoja na kero za wananchi iliyofanyika katika eneo la wazi la Kanisa la TAG, Mtaa wa Nganza, Kata ya Luchelele Jijini Mwanza.
Amesema migogoro ya ardhi imekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa kuwa maeneo yenye migogoro hushindwa kuvutia uwekezaji na maendeleo ya miundombinu muhimu.
“Kama hatutamaliza migogoro ya ardhi hatuwezi kupanga maendeleo, lazima tufike mahali tuseme migogoro sasa basi,” amesema Mhe. Mtanda.
Aidha amewataka watumishi wa sekta ya ardhi kutokuwa chanzo cha migogoro huku akionya kuwa ucheleweshaji wa ulipaji wa fidia ya maeneo yaliyotwaliwa na Halmashauri umekuwa ukichochea migogoro.
Mhe. Mtanda amesema viongozi wanaweza kubadilika lakini migogoro itaendelea kuwepo kama wananchi hawatakuwa na utashi wa kweli wa kutafuta suluhisho la kudumu kwa njia ya mazungumzo na maridhiano.
“Hapa hatupo kunyoosheana vidole, tumefika mahali ambapo lazima pande zote zikae chini na kukubaliana ili maendeleo yaendelee,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
May 19, 2026
Rating:



No comments: