Waandaaji wa shindano la Miss Tanzanite 2025 chini ya Mkurugenzi wa shindano hilo, Aminatha Shamghe, wamesema mshindi wa taji hilo, Rachel Adam Nziku, anawakilisha zaidi ya uzuri wa sura kwa kuwa ni kielelezo cha maadili, kujiamini na uthabiti wa mwanamke wa Kitanzania.
Katika taarifa yao, waandaaji hao wamesema walipoanza mchakato wa kumtafuta Miss Tanzanite 2025 hawakuwa wanatafuta uzuri pekee, bali mtu anayebeba roho na thamani halisi ya madini ya Tanzanite ambayo ni alama ya kipekee ya Tanzania.
Wamesema Rachel si mtu anayependeza mbele ya kamera pekee, bali anadhihirisha neema, kusudi na kujiamini katika kila hatua anayopiga, hali inayomfanya kuwa balozi bora wa wanawake wa Kitanzania.
“Rachel habebi taji tu, bali anawakilisha uthabiti, ukarimu na mwangaza wa mwanamke wa Kitanzania. Ni ukumbusho kwamba heshima ya kweli ya uongozi na ufalme hutokana na nguvu ya tabia na utu wa mtu,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Waandaaji hao wameongeza kuwa ushindi wa Rachel unaashiria mwanzo wa enzi mpya ya vijana wenye maono, maadili na dhamira ya kutumia majukwaa yao kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Aidha, wamemkaribisha rasmi katika safari ya kuitumikia jamii kupitia taji hilo, wakieleza kuwa wanajivunia kuwa sehemu ya safari yake ya mafanikio na maendeleo.
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
June 23, 2026
Rating:





No comments: