Wanachama na wananchi wa Kata ya Nangara, Babati Mjini, leo wameendelea na siku ya pili ya ziara ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Babati Mjini, Bi Elizabeth Malley, ambapo malengo makuu ya ziara hiyo ni Kuimarisha Chama mashinani.
Katika mkutano wake na viongozi wa matawi na wanachama, Bi Malley amegusia maeneo makuu matano:
*Kwanza, Uhai wa Chama.* Mwenyekiti amesisitiza umuhimu wa kuongeza wanachama wapya, kulipa ada kwa wakati na kufanya vikao vya chama kwa mujibu wa Katiba na kanuni. Amesema chama imara ni chenye nidhamu na kinachofuata taratibu.
*Pili, Utekelezaji wa Ilani ya CCM.* Bi Malley amempongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuleta fedha nyingi za maendeleo katika nyanja mbalimbali kama elimu, afya, maji na miundombinu. Naye Diwani wa Kata ya Nangara alipata nafasi ya kueleza utekelezaji wa Ilani katika mitaa yote ya kata hiyo.
*Tatu, Kusikiliza na Kutatua Kero za Wananchi.* Wananchi walipata nafasi ya kueleza kero mbalimbali zinazowakabili, ambapo baadhi ya kero hizo zilijibiwa papo hapo na zingine zimebeba kwa ajili ya kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Babati.
*Nne, Miradi ya Chama.* Mwenyekiti alieleza umuhimu wa Chama kuwa na miradi yake ya kiuchumi ili kujiendesha. Aidha, alizungumzia mpango wa ujenzi wa Ofisi za Chama katika Matawi na Kata, kama sehemu ya kuimarisha uwepo wa CCM mashinani.
*Tano, Amani na Mshikamano.* Amesisitiza kudumisha amani, umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama na wananchi wote, akisema bila amani hakuna maendeleo.
Ziara ya Mwenyekiti inaendelea katika kata nyingine za Babati Mjini kwa lengo moja la kukisogeza Chama karibu zaidi na wananchi.
--
Reviewed by VISION MEDIATZBLOG
on
September 22, 2026
Rating:





No comments: